NA ANDREW CHALE,
VIJANA wa Kitanzania wabunifu katika teknolojia wa kampuni ya See Different Experiences (SEEDE) wamebuni bidhaa ijulikanayo kama C-section VR Training Simulation ambayo itamwezesha Daktari ama mtaalam wa Kada ya Afya kujifunza na kufanya upasuaji wa kujifungua Mama mjamzito kwa njia ya kisasa kwa kutumia vifaa maalumu (VR headsets).
Akizungumza wakati wa utambulisho wa mpango huo kwa Wadau mbalimbali Jijini Dar es Salaam, tukio lililoandaliwa na Ona Stories Group ambao imewavumbua na kuwalea kitaaluma Vijana hao, Bernard Masika wa SEEDE, amesema waliamua kutumia fursa ya teknolojia ya kisasa ya uhalisia pepe ‘virtual reality’ ilikuboresha mafunzo ya sekta ya afya.
“SEEDE tumefanikiwa kuonesha kuwa linawezekana, kwa kufanikiwa kutengeneza moja ya toleo la mwanzo kabisa (MVP – Minimum viable product) la bidhaa yao ijulikanayo kama C-section VR Training Simulation.
Hii itaenda kuvunja minyonyoro ya changamoto za kujifunza na kufanya upasuaji wa kujifungua mama mjazito.” Amesema Bernard Masika.
Aidha, ameongeza kuwa kwa kutumia vifaa hivyo maalumu vya VR, Mwanafunzi wa Udaktari au Daktari mwenyewe, ataweza kufanya operesheni hiyo katika mazingira kama ya kweli (immersive experience)
Ambapo itamruhusu kufanya makosa, na kujirekebisha kutoka kwenye makosa hayo lakini pia itaweza kumpa alama (marks) na maoni mwishoni mwa kila upasuaji unavyofanyika.” Amemalizia Bernard Masika.
Kwa upande wake, Daktari bingwa wa magonjwa ya Akinamama kutoka Hospitali ya Agha Khan, Dkt.Jane Muzo amepongeza Vijana hao wagunduzi pamoja na Ona stories Group kuwa, Tanzania inaenda kuwa Nchi ya kwanza Duniani kuja na ubunifu huo ambao utakuja kuwa msaada endelevu kwa Taifa.
Ameweka wazi kuwa, mpango huo kukamilka kwake unaenda kupunguza vifo vya akinamama vitokanavyo na uzazi pingamizi ikiwemo kujifungua kawaida ama kwa upasuaji na hata pia kuokoa vifo vya watoto hapa nchini.
‘’Hii bidhaa itasaidia na kuleta manufaa katika jamii yetu kuokoa maisha ya akina mama.
Lakini pia kupunguza vifo vya wazazi kutokana na kutokupata huduma vizuri za kujifungua kwa njia ya upasuaji.” Amesema Dkt. Jane Muzo.
Na kuongeza kuwa, huduma hiyo inaweza kufika hata sehemu ambazo hazikufikiwa ukiacha mjini ambapo kila kitu kipo, lakini pia Vijijini vitafikiwa na hii huduma kwa haraka zaidi.
“Madaktari ambao hawajawahi kupata uzoefu au kuona operesheni inafanyikaje, wataweza kupata ujuzi wa kufanya upasuaji vizuri, itawapa elimu zaidi kwani itakuwa ni sawa na karibia ya asilimia 100 ya uwepo wao wa sehemu ya chumba cha upasuaji na mwisho wa siku tutapata wataaluma wengi ambao watakuwa na ubunifu mzuri na kupunguza madhara yatokanayo na kutofanya upasuaji vizuri kwa mama zetu ambao wanastahiri kufanyiwa upasuaji, mama zetu watakuwa salama na watoto wetu watakuwa salama.” amemalizia Dkt. Jane Muzo.
Aidha, amesema kuwa, yupo tayari kuwapa ushirikiano akiwa kama Daktari huku akitoa wito wadau kuwashika mkono Vijana hao.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni ya Ona Stories, Princely Glorious amesema kuwa wanajisikia faraja kuwa miongoni mwa waliowavumbua Vijana hao kupitia mashindano ya AR /VR Africa Metathon (Meta+hackathon) yaliyofadhiliwa na kampuni ya Meta inayosimamia mitandao ya Factbook, Whatsapp na Instagram) kwa kuratibiwa na Imisi 3D ya Nigeria kwa ushirikiano na Black Rhino’s kutoka Kenya ambapo Ona Stories walikua wenyeji wa hayo mashindano kwa Tanzania na kuweza kutoa mshindi bora kati ya nchi 16 zilizoshiriki Bara la Afrika.
‘’Ona Stories kupitia teknolojia hii ya Uhalisia pepe ni teknolojia bunifu na tunajivunia vijana wa SEEDE kwani mpango wao huo unaenda kuwa msaada mkubwa kwa Taifa.
Lakini pia tumepokea kwa furaha kubwa ubunifu huu, tuendelee kuwashika mkono vijana hawa ikiwemo mahitaji vifaa, fedha na mambo mbalimbali ilikuendelea kukuza ubunifu wao’’ amesema Princely.
Kampuni hiyo ya SEEDE inaundwa na Vijana watano ambao ni Bernard Masika, Judith Solomon, Shabo Andrew Fredrick Mallya na Alex Mkwizu huku wawili Judith na Alex wakiwa bado wanaendelea na Chuo Ndaki ya Tehama Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na wengine watatu walishahitimu vyuo tofauti tofauti hivi karibuni.