Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kipindi cha kuanzia Aprili Mosi hadi 11, 2023 limefanya Misako na Doria za nguvu na zenye tija katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya na kupata mafanikio makubwa ikiwemo kukamata watuhumiwa 44 kati yao wanaume ni 41 na wanawake 03 wakiwemo watuhumiwa wa mauaji, unyang’anyi wa kutumia silaha, kuvunja nyumba usiku na kuiba, utapeli, wizi wa mifugo na kupatikana na dawa za kulevya na pombe haramu ya Moshi @ Gongo.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa wawili kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha na utekaji wa magari katika eneo la Mlima Msangamwelu barabara ya Mbeya – Mkwajuni Wilaya ya Chunya.
Awali Machi 23, 2023 majira ya saa 07:30 usiku huko maeneo ya Mlima Msangamwelu Wilaya ya Mbeya Vijijini katika barabara kuu ya Mbeya – Mkwajuni, Watuhumiwa wakiwa na wenzao wanne wakiwa na silaha mbalimbali waliweka magogo kwenye barabara na kuteka magari mawili yaliyokuwa yakitokea Mkwajuni kuelekea Mji Mdogo wa Mbalizi yakiwa yamebeba bidhaa mbalimbali pamoja na wafanyabiashara.
Watuhumiwa walipora fedha taslimu na vitu mbalimbali vya wafanyabiashara hao vyote vikiwa na thamani ya Tshs. 11,190,000/= zikiwemo simu za mkononi, mabegi na kisha kutolewa kusikojulikana. Baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi lilianza ufuatiliaji na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili. Upelelezi unaendelea.
Aidha katika muendelezo wa misako, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanikiwa kumtia mbaroni kijana wa kiume CLAUD ALEX MWINUKA [22], Mkazi wa Mbugani wilaya ya Kyela kwa tuhuma za kuruhusu kuingiliwa kinyume cha maumbile kwa kuwalaghai na kuwashawishi wanaume katika maeneo ya Bar na kumbi za Starehe.
Mtuhumiwa alikamatwa Aprili 05, 2023 huko Wilaya ya Kyela na katika uchunguzi wa awali uliofanywa na madaktari wa Hospitali ya Wilaya hiyo, ilibainika kuwa sehemu ya nyuma ya maumbile ya mtuhumiwa imeingiliwa na kitu kigumu.
Aprili 06, 2023, mtuhumiwa alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Kyela na kusomewa shitaka lake kwa kosa la kuruhusu kuingiliwa kinyume na maumbile katika kesi ya jinai namba 39/2023 chini ya kifungu namba 154 (1) [C] cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Mtuhumiwa alikiri kutenda kosa hilo na Mahakama kumtia hatiani kutumikia kifungo jela miaka 30.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia ZAWADI SASTONI @ NZUNJE [30] Mkazi wa Igalako Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya kwa tuhuma za kumuua mtoto wake wa kambo aitwaye MESHAKI FAZILI @ MLAWA [12] Mkazi wa Kapyo kwa kumpiga kwa kitu kizito kichwani na kukimbia kusikojulikana.
Awali Aprili 02, 2023, mtuhumiwa alitoweka nyumbani kwake akiwa na mtoto huyo kwenda naye kusikojulikana ambapo Aprili 04, 2023 ilifunguliwa kesi ya wizi wa mtoto katika kituo cha Polisi Igurusi. Kutokana na tukio hilo, tulianza msako mkali na Aprili 06, 2023 tulimkamata mtuhumiwa.
Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hili ni mgogoro kati ya mtuhumiwa na mke wake ambao ulipelekea chuki na hasira dhidi ya mtoto huyo ndipo mtuhumiwa akapanga kumuua mtoto huyo ili kumkomoa aliyekuwa mke wake. Upelelezi unaendelea na mara baada ya kukamilika atafikishwa mahakamani.
Sambamba na hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa nane [08] kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya kuvunja nyumba usiku na kuiba, kuvunja ofisi usiku na kuiba na kuvunja magodauni usiku na kuiba mali mbalimbali.
Watuhumiwa baada ya kupekuliwa walikutwa na mali/vitu mbalimbali vya wizi ambavyo ni:-
TV Flat Screen 03 aina ya Star X, Alyons na Samsung
Radio 03 aina ya Sundar
Camera 01 aina ya Sony
Radio Sub-woofer
Magodoro matatu.
Simu za Mkononi 03
Remote Control 01
Solar Panel 01 aina ya Sundar
King’amuzi cha Star Times
Twitter 03 za Radio aina ya Sea Piano, Aborder na Sundar
Beseni la Plastic
Monitor 01, Mouse 01, Wifi Router na Hard Disk 02.
Mifuko 02 ya Mbolea ya kilogramu 50 kila mmoja.
Pasi 02 aina ya Tronic
Mashine 01 ya kutengenezea chapati
Rice Cooker 02 aina ya Mammo Nlex
Seti 02 ya Hot Pot aina ya Soltaire
Majiko ya Gesi
Vitanda vya kulalia.
Nguo za aina mbalimbali.
Vifaa vya kupikia kama vile masufuria
Majagi ya kuchemshia maji.
Aidha katika tukio hili, amekamatwa mtuhumiwa mmoja mwanamke mkazi wa Mji Mdogo wa Tunduma Mkoa wa Songwe ambaye ni mpokeaji na mtunzaji wa mali za wizi. Baadhi ya mali/vitu hivyo vimeanza kutambuliwa na wahanga, tunaendelea kutoa rai kwa wananchi kufika vituo vya Polisi kwa ajili ya utambuzi na kurejeshewa mali zao kwa mujibu wa taratibu pamoja na kutoa ushahidi mahakamani ili kesi zipate mafanikio.
Vile vile, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na mapambano dhidi ya dawa za kulevya na katika kipindi cha kuanzia Aprili 01 hadi 11, 2023 tumefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 20 kwa tuhuma za kupatikana na dawa za kulevya aina ya bhangi ambapo jumla ya kilogramu 15.62 ilikamatwa. Aidha watuhumiwa wamekuwa wakijihusisha na ulimaji, uuzaji na matumizi ya dawa hizo.
Pia tunawashikilia watuhumiwa 06 kwa tuhuma za kutengeneza, kuuza na kutumia pombe haramu ya Moshi @ Gongo. Watuhumiwa kwa Pamoja walikamatwa wakiwa na kiasi cha lita 46 ya pombe hiyo haramu.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa jamii kupiga vita vitendo vya ushoga/mapenzi ya jinsia moja kwani ni kinyume cha sheria pia maadili ya Mtanzania. Aidha tunatoa wito kwa wana ndoa kutatua migogoro yao kwa kushirikisha wazazi, walezi na viongozi ili kupata suluhu ya mambo yao.
Imetolewa na:
BENJAMIN E. KUZAGA – ACP
Kamanda wa Polisi,
Mkoa wa Mbeya.