Jumuiya ya Umoja wa vijana wa chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Njombe UVCCM imekiri kutumia ripoti ya CAG kuanza uchunguzi kwa watumishi wa umma waliofanya ubadhirifu katika taasisi za serikali na miradi ya umma mkoani huko utakaochukua wiki mbili na Kisha kutoa ushauri na maelekezo juu ya hatua za kuchukuliwa kwa wahusika .
Awali Hamis Kachinga ambaye ni katibu wa Jumuiya ya Umoja wa vijana wa chama Cha Mapinduzi UVCCM mkoa wa Njombe ,wakati wakizindua kampeni ya nasimama na mama itakayohusisha makundi mbalimbali katika jamii wakiwemo viongozi wa dini,wasanii,wafanyabiashara na waandishi wa habari yenye Lengo la kueleza mambo yaliyofanywa na serikali sambamba na kutoa elimu ya ujasiriamali,mikopo na masoko amesema wanakwenda kuanika mbivu na mbichi kuhusu ubadhirifu baada ya wiki mbili.
“Kuna ubadhirifu umefanywa na watumishi wa serikali sisi Kama Jumuiya tunakwenda kuchunguza hili na ndani ya wiki mbili tutakuwa tumejua na tutawaita wanahabari tuwape majibu “alisema katibu UVCCM mkoa wa Njombe Hamis Kachinga.
Kuhusu suala la maadili na fursa Mwenyekiti UVCCM mkoani humo Samwel Mgaya amesema katika kampeni hiyo watatumia mikutano na MIDAHALO kuelimisha juu ya athari za mmomonyoko wa maadili na Kisha kutoa onyo kwa wana-CCM ambao wanaendekeza uchawa kwa viongozi ili wapate kula na madaraka badala la kuchapa kazi kwa bidii ili watambulike kwa uwezo wao.
Mgaya amesema katika kampeni hiyo watashirikiana na wataalamu wa serikali kutoa elimu ya mikopo,ukatili wa jinsia na Kisha kueleza makakati wa ununuzi wa mabasi mawili ya Jumuiya hiyo ambayo yatakuwa yakifanya safari zake wilayani Makete Lengo likiwa ni kuunga mkono jitihada za rais Samia za kuwaletea maendeleo Watanzania.
“Tunakwenda kuzindua kampeni kubwa iliyopewa jina nasimama na mama itakayohusisha makundi tofauti katika jamii ,ikiwa na dhamira nyingi ndani yake ikiwa ni pamoja na kupinga UKATILI wa kijinsia na mmomonyoko wa maadili”alisema Samwel Mgaya Mwenyekiti wa UVCCM Njombe.