Waziri wa Mambo ya Nje na Ushikirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Stergomena Tax amesema kwamba ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris aliyoifanya mwishoni mwa mwezi Machi nchini Tanzania imeleta mafanikio makubwa.
Akizungumza leo na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam Waziri Tax amesema kwamba ziara hiyo imesababisha mafanikio mbalimbali ikiwemo Serikali ya Marekani kuahidi kujenga kiwanda kikubwa cha kipekee Barani Afrika cha kuchakata Madini yanayotumika kutengeneza betri za gari za umeme kwa ajili ya Soko la Marekani na Dunia kwa ujumla.
Amesema kwamba ujenzi wa kiwanda hicho cha kuchakata Madini ya Kutengeneza betri za gari za Umeme unatarajiwa kukamilika mwaka 2026 ambapo utasaidia kutoa ajira kwa Watanzania nakukuza Pato la Taifa.
Amendelea kufafanua kuwa Mkataba mwingine uliosainiwa kati ya Marekani na Tanzania ni ule unaohusu Msaada wa maendeleo kati ya nchi hizo mbili ambapo zaidi ya Dola za kimarekani bilioni 1 ili kutekeleza miradi ya kijamii na kiuchumi.
Aidha Mradi mwingine nikuhusu masuala ya Tehama ili kuwezesha kuboresha mfumo wa mawasiliano kuwa wa teknolojia ya kisasa wa 5G,mapambano dhidi ya uhalifu wa kimtandao na usalama wa kimtandao ili kuhakikisha nchi inakua salama katika nyanja mbalimbali ikiwemo sekta ya kiuchumi.
Waziri Tax pia amendelea kusema kwamba mkataba mwingine niwa kuwezesha serikali ya Marekani kutoa ushauri wa Kitaalamu kuhusu usimamizi wa Bandari za Tanzania ususani katika usimamizi wa Bandari pamoja na matumizi ya vifaa vya kisasa na upanuzi wa Bandari.
Makamu wa Rais Wa Marekani Kamala Harris aliwasili nchini Tanzania Machi 29 ,2023 nakuweza kutembelea makumbusho ya Taifa nakuweka shada la maua kwa kuwakumbuka wahanga wa shambulio la kigaidi lililotokea mwaka 1998 katika ubalozi wa marekani nchini Tanzania.
Katika hatua nyingine Waziri Stergomena Tax amekutana na mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini Tanzania nakuwaeleza hatua zilizochukuliwa na serikali katika kukabiliana na ugonjwa wa marburg ambao umegundulika mkoani Kagera nakusababisha visa 8 vya ugonjwa huo huku watu 5 kati yao walifariki dunia,wengine 3 kuendelea kupatiwa matibabu.
Aidha amewahakikishia Mabalozi hao kuwa Tanzania ni nchi salama kutokana na serikali kupitia Wizara ya Afya kufanikiwa kuudhibiti ugonjwa huo huku akiwaomba raia wa nchi zao kuwaruhusu raia wa nchi zao kuja nchini Tanzania.