Na Mwandishi wetu, Mirerani
WANAWAKE wadau wa madini ya Tanzanite wa Tarafa ya Moipo, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wametakiwa kutolalamikia changamoto zinazowakabili ila waeleze mbinu za kuwaondoa na kuwaingiza kwenye fursa.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Dk Suleiman Serera ameyasema hayo wakati akizungumza na wanawake wajasiriamali, wanunuzi wa madini, magonga, wauza maziwa, vyakula na matunda, ndani ya ukuta wa madini ya Tanzanite.
Dk Serera amesema wanawake hao wanapaswa kuelezea mbinu na njia za kuwatoa kwenye changamoto wanazoziona zinawakabili mara kwa mara na siyo kulalamika kila wakati.
“Wanawake ni jeshi kubwa hivyo mnapaswa kupambana kwa kuonyesha njia ya kuondokana na changamoto zilizopo mbele yenu na siyo kulalamika juu ya vikwazo mbalimbali,” amesema Dk Serera.
Amelipongeza shirika la lisilo la kiserikali la Civil Society Protection Foundation (CSP) kwa kufanya mdahalo na kuwakutanisha wadau wa madini ya Tanzanite ili kutafuta mbinu za kuondokana na changamoto.
Mkurugenzi wa CSP, Nemency Iriya amesema waliandaa mradi wa Tanzanite na uchumi imara wa mwanamke, unaotarajia kunufaisha kata tatu za Mirerani, Endiamtu na Naisinyai.
Iriya amesema mradi huo umelenga kuhakikisha wanawake wajasiriamali wanaofanya biashara zao ndani ya ukuta unaozunguka migodi hiyo wanafanya kazi zao kwa ufanisi.
“Tunatarajia wanawake hao watafanya biashara zao kwa amani, uhuru na faida, kwani mara baada ya kujengwa ukuta unaozunguka migodi ya Tanzanite kumekuwa na changamoto zinazowakabili,” amesema.
Mmoja wa wadau hao, Mwanaidi Kimu alisema wanawake wa umri mkubwa wanaamriwa kuvua nguo ya ndani na askari wa umri mdogo ili kupekuliwa na kusababisha ukatili wa kijinsia.
“Japokuwa baadhi ya wanawake ndiyo wamesababisha hali hiyo kwa kufanya vitendo viovu kwa kufisha madini kwenye tupu zao ila serikali iweke vifaa vya kutupekua,” amesema Kimu.
Mwanamke mwingine, Hawa Kiranga amesema wanawake wajasirimali wanaouza vyakula, matunda na maziwa, ndani ya ukuta hawaruhusiwi kutoa nje pindi vikibaki.
“Tunaomba serikali ifanye mpango wajasiriamali waruhusiwe kutoka na vyakula vyao jioni endapo vikibaki ili watoto wao wakale nyumbani, kuliko kumwaga na kupata hasara,” amesema Kiranga.