Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Epheta Edward akimpima wingi wa sukari mwilini mkazi wa Iringa Magreth Sanga wakati wa kambi maalum ya siku tano ya uchunguzi na matibabu ya moyo inayofanywa na wataalam wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa.
Mtafiti wa Taasisi ya Moyo jakaya Kikwete (JKCI) Makrina Komba akimuuliza maswali ya ufahamu kuhusu magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo mkazi wa Iringa Christina Chibona kabla ya kufanyiwa uchunguzi na matibabu ya moyo wakati wa kambi maalum ya siku tano inayoendelea katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa.
…………………….
Na: Genofeva Matemu – Iringa
06/04/2023 Wananchi wa Mkoa wa Iringa wameishukuru Serikali ya awamu ya sita kupitia Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kuwezesha huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya moyo kuwafikia kwa karibu kwani wananchi wengi hawana uwezo wa kufuata huduma za kibingwa mahali zilipo.
Pongezi hizo zimetolewa na wananchi mbalimbali waliofika katika kambi maalum ya siku tano ya matibabu ya moyo inayoendelea katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa (IRRH).
Akizungumza baada ya kupatiwa matibabu ya moyo mkazi wa Iringa Mzee Nicholas Kinyamagoha alisema hakuwahi kufanya uchunguzi wa moyo wake tangu kuzaliwa kwake kutokana na huduma hizo kuwa mbali na sehemu anayoendesha maisha yake.
Mzee Nicholas alisema baada ya kusikia ujio wa madaktari bingwa wa moyo Mkoani Iringa akaona ndio fursa pekee anayoweza kutumia kuchunguza moyo wake kwani kutokana na umri wake kuwa zaidi ya miaka 60 yupo katika hatari ya kupata magonjwa mbalimbali yakiwemo magonjwa ya moyo.
“Nashukuru leo nimefika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa na kupata fursa ya kupimwa moyo wangu, awali walishangaa kuona shinikizo langu la damu kuwa juu lakini baada ya kuwaeleza taarifa mbaya niliyopokea wakati nikiwa kwenye foleni kusubiri matibabu walinipa muda wa kupumzika na kuchunguzwa tena shinikizo langu la damu”, alisema Mzee Nicholas.
Mzee Nicholas alisema ikiwezekana huduma za uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza ambayo sio rahisi kuyapata katika Hospitali zilizopo mikoani ziwe zinatolewa angalau mara moja kwa mwaka ili wananchi wapate nafasi ya kutibiwa kwa wakati pale wanapokutwa na magonjwa hayo.
“Nimefurahi sana leo nimepima moyo wangu kwa mara ya kwanza, nimeweza kujua namna ya kujikinga ili nisipate magonjwa ya moyo na nimesisitizwa nisiache kutumia dawa za shinikizo la damu ambazo nimekuwa nikizitumia kwa miaka miwili sasa”, alisema Mzee Nicholas.
Akizunguma kwa nyakati tofauti mkazi wa Iringa Felister Chang’a alisema mwaka 2020 alikuwa na dalili za kupumua kwa shida, maumivu makali upande wa kushoto wa kifua yaliyoenda hadi mgongoni hivyo kufika katika moja ya Hospitali zilizopo Iringa na kupimwa moyo lakini majibu yalitoka kuwa hana shida ya moyo.
Felister alisema baada ya uchunguzi aliofanyiwa mwaka 2020 alipewa dawa za maumivu na kuendelea na maisha lakini mwaka huu zile dalili zimerudi na hakuwa na chakufanya kwani hapo awali alishaambiwa sio shida ya moyo.
“Niliposikia ujio wa madaktari bingwa wa moyo kutoka JKCI kwakweli nilifurahi sana kwani naamini leo naenda kupata suluhu ya tatizo nililinalo kwasababu ninapopata maumivu ya kifua na kushindwa kupumua kunanifanya nishindwe hata kufanya shughuli zangu”, alisema Felister.
“Jana nilimleta mtoto wangu hapa kwa ajili ya kutibiwa, baada ya kufika hapa nikaona bango linaloonyesha uwepo wa madaktari bingwa wa moyo nikakumbuka mimi pia nahitaji kumuona daktari wa moyo kutokana na hali yangu ya maumivu ya kifua, nashukuru sijakutwa na shida ya moyo wameweza kunichunguza na kuona tatizo la vidonda vya tumbo”, alisema Felister.
Akiongea kwa furaha Felister amewashukuru Madaktari bingwa wa moyo kwa kuona umuhimu wa kuwafikia wananchi wa Iringa kwani bila ya wao kufika asingejua kama maumivu anayoyapata yanasababishwa na vidonda vya tumbo.
Naye mkazi wa Songea aliyesafiri kufuata huduma za matibabu ya moyo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa Zamda Bakari alisema baada ya kusikia ujio wa madaktari bingwa wa moyo hakuona shida kusafiri kutoka Songea kufuata huduma hiyo kwani amekuwa akihitaji kuchunguza moyo kwa muda mrefu.
“Nilimpoteza baba yangu kwa kifo cha ghafla na baada ya kufuatilia tuliambiwa alipata shambulio la moyo hivyo kumsababishia kupata kifo cha ghafla, baada ya kifo cha baba yetu nimekuwa makini nikisikia huduma za kibingwa za uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza nawiwa kuchunguza afya yangu ili nijitambue”, alisema Zamda.
Zamda aliwashauri wananchi wanzake kupima afya zao mara kwa mara pale wanapopata nafasi kwani kumpoteza mtu wa karibu kwa kushindwa kujua kama alikuwa anaumwa inaumiza.