Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi leo Aprili 6, 2023 ametembelea na kufanya mazungumzo na menejimenti za Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) katika ofisi zao mjini Morogoro.
Katika vikao hivyo Katibu Mkuu amewataka viongozi hao kuendana na kasi ya sasa ya Wizara
inayoongozwa na Mhe. Waziri Mohammed Mchengerwa chini ya
maono mapana ya Rais Samia Suluhu Hassan kupitia filamu ya Royal Tour.
“Kwa sasa Wizara inazingatia falsafa mbili za Wizara ambazo ni Uhifadhi (Conservation) na Kutangaza (Promotion) kwa vivutio na maliasili zetu hivyo kazi zenu zote zizingatie hayo,” alisema Dkt. Abbasi.
Akihitimisha vikao hivyo, Dkt Abbasi amewaasa viongozi hao kuwa watendaji wazuri, kuzingatia maadili ya kazi na kuhakikisha watumishi wa taasisi hizo wanapata stahiki zao na kila mtu anafanya kazi kwa furaha.
“Kuweni watekelezaji, msiwe watu wa maneno mengi bila vitendo, tunataka kazi zenye matokeo ya haraka na wafanyakazi waone wanafarijiwa vyema ili kuongeza ufanisi,” alisisitiza.