……………….
Na Muhidin Amri,
Newala
ZAIDI ya wakazi elfu ishirini wa vijiji 13 katika jimbo la Newala mjini mkoani Mtwara,wanatarajia kuondokana na kero ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama baada ya serikali kutoa zaidi ya Sh.bilioni 2.326 kutekeleza mradi wa maji Mnaida.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo kwa kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2023 Abdala Shaibu Kaim, Meneja wa Ruwasa wilayani Newala Mhandisi Sadik Msajigwa amesema,mradi huo ulianza kutekelezwa mwezi April na kutakiwa kukamilika mwezi Oktoba mwaka 2022.
Kwa mujibu wa Msajigwa,hata hivyo mkandarasi aliongezewa muda wa utekelezaji hadi tarehe 30 Oktoba 2023 kutokana na kuchelewa kwa fedha za utekelezaji wa mradi huo na kutopatikana kwa msamaha wa kodi ndani ya muda.
Alisema,hadi sasa mkandarasi ameshalipwa jumla ya Sh.milioni 366,499,902.61 na mradi umefikia asilimia 85 ya utekelezaji wake ambapo mkandarasi yuko hatua ya mwisho ya umaliziaji kwa kujenga vituo vya kuchotea maji(DPS) na ujenzi wa teki la lita 225,000.
Alieleza kuwa,miundombinu ya mradi huo itasaidia sana kuunganisha huduma ya maji kwa zaidi ya wakazi 20,546 wanaoishi katika vijiji vya Mnaida,Msilili,Lidumbe Mcholigodauni,Chiwindi na vijiji vingine vilivyopo kata ya Lidumbe na Mkunya.
Msajigwa,ameishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zilizofanikisha kuanza utekelezaji wa mradi huo kwani utaongeza chachu ya maendeleo kwa kupunguza muda wa kutafuta maji hasa kwa akina mama na watoto na kutimiza adhima ya Rais Samia ya kumtua mama ndoo kichwani.
Alisema kuwa,awali wakazi wa vijiji hivyo walilazimika kuamka usiku kati ya saa nane na saa kumi usiku kwenda kutafuta maji umbali wa zaidi ya kilomita 9.5 yanayopatikana kwenye mabonde na milima.
Kwa upande wake Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2023 Abdala Shaibu Kaim,amewapongeza wataalam wa Ruwasa kusimamia vyema mradi huo na viongozi wa mkoa wa Mtwara kwa jitihada kubwa wanazofanya katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi ikiwemo ya maji.
Amewataka wananchi wa jimbo la Newala mjini,kuhakikisha wanatunza mradi huo na miundombinu yake ili mradi wa maji Mnaida uweze kudumu kwa muda mrefu na kumaliza changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo katika maeneo yao.
Mkuu wa wilaya ya Newala Rajabu Kundya alisema,tatizo la maji katika wilaya hiyo ni kubwa na la muda mrefu na hali hiyo imetokana na mji wa Newala kuwa juu zaidi ya mita 800 kutoka usawa wa Bahari,kwa hiyo ni vigumu kupata suluhuhisho la kudumu la huduma ya maji safi na salama kwa wananchi.
Hata hivyo,amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuiangalia kwa jicho la pili wilaya hiyo na kuipatia fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji katika maeneo mbalimbali.