Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko akizindua Kalenda ya Mafunzo kwa Wachimbaji Wadogo na kushuhudia Utiaji Saini Makubaliano ya kuwasaidia wachimbaji wadogo baina ya STAMICO na Taasisi za Fedha na Wauzaji wa Vifaa vya uchimbaji ili kuweza kuwasaidia wachimbaji wadogo Kushoto ni Mwenyekiti Wa Bodi ya Wakurugenzi Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Meja Jenerali Mstaafu Michael Isamuhyo.
………………………………
Na Anjela Seth
Waziri wa Madini Dotto Biteko amewataka wamiliki wa viwanda vinavyozalisha bidhaa kwa kutumia madini kununua madini hayo kutoka kwa wachimbaji wadogo wadogo wa madini kwa bei elekezi ya serikali.
Pia ameitaka Tume ya Madini kwa kushirikiana na Shirika la Madini la Taifa( STAMICO) kuhakikisha wanatoa fursa kwa vijana,wanawake na Watu wenye Ulemavu waweze kupata vitalu na kufanya kazi za uchimbaji wa madini ya viwandani hali itakayowasaidia kujikwamua kiuchumi nakuacha kulalamika.
Waziri Biteko ametoa maelekezo hayo leo Jijini Dar es salaam wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa siku mbili uliowakutanisha wachimbaji wadogo wa madini,Wamiliki wa Viwanda,Sekta za kifedha pamoja na wadau wengine wa sekta ya madini kwa ajili ya kujadili changamoto zinazowakumba wachimbaji wadogo w madini nakuzipatia ufumbuzi.
“Wapatieni fursa wanawake na watu wenye Ulemavu hata kama hawana mitaji watachimba madini kwa kuingia ubia na makampuni mengine ili waache kulalamika,hivyo tuendelee kutoa vifaa vya kuchimbia kwa gharama nafuu kwa walemavu ili tuwainue kiuchumi” amesema Waziri Biteko
Aidha amesema kwamba serikali imeweka lengo la kuchangia asilimia 10 ya pato la Taifa kupitia sekta ya Madini ifikapo 2025, ambapo kwa sasa Sekta hiyo inachangia kiasi cha Trioni 1.19,hivyo ili kufikia lengo ni lazima kuweka mazingira rafiki ya kufanya shughuli za uchimbaji wa madini ikiwemo mifumo mizuri ya kodi,kuwapatia mikopo pamoja nakuwa na masoko ya uhakika.
Hata hivyo amesisitiza Wachimbaji wadogo wa madini ya viwandani kuzingatia ubora wa malighafi ili kuwafanya watu wenye viwanda hapa nchini waweze kununua malighafi hizo nakusaidia kuzalisha bidhaa kwa gharama nafuu nakuweza kukuza Uchumi wa Taifa.
Aidha Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt Venance Mwasse amesema kwamba mkutano huo unalengo la kujadili kwanini viwanda vya hapa nchini havitumii malighafi zinazopatikana hapa nchini nakuweza kutafuta ufumbuzi ili kuvifanya viwanda hivyo viweze kutumia malighafi hizo nakuwafanya wachimbaji hao wakue kiuchumi na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake rais wa Wachimbaji wa Madini Jonh Bina amesema kwamba wachimbaji hao wanakumbwa na changamoto lukuki zinazohitaji ufumbuzi wa haraka huku akizitaja baadhi kuwa ni pamoja na Kukosekana kwa mitaji ya uhakika,tozo kubwa ya kodi ya ongezeko la thamani( VAT), Kupanda kwa bei ya makaa ya mawe,nakuiomba serikali kutatua changamoto hizo mapema iwezekanavyo ili kuifanya Tanzania kuwa sehemu ya amani yenye fursa za masoko ya madini.
Halikadhalika Mwakilishi wa watu wenye Ulemavu kwenye Mkutano huo Mbunge wa Viti Maalumu Riziki Lulinda ameishukuru serikali kupitia Wizara ya Madini kutoa kipaumbele kwa watu wenye Ulemavu ili waweze kushiriki katika shughuli za uchimbaji wa madini nakuweza kujipatia kipato cha kuendesha maisha yao pamoja na kukuza uchumi wa Taifa.
Zaidi ya Washiriki 700 kutoka sekta madini wamehudhuria mkutano huo wa muhimu kwa ajili ya kujadili changamoto zinazowakumba wachimbaji wadogo wa madini,wamiliki wa viwanda pamoja na wanunuzi wa madini ili kuweza kuzipatia ufumbuzi nakukuza sekta ya Madini nchini.