Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB), John Maige akisaini mkataba na Mkurugenzi wa KPMG, Adolf Boya Kushoto.
………………………
Na Selemani Msuya
BODI ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB), imesaini mkataba wa Sh.milioni 200 na Kampuni ya KPMG kwa ajili ya kuandaa mpango mkakati wa bodi hiyo ambao utekelezaji wake utaanza Julai 2023 hadi 2028.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CPB, John Maige wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, ambapo aliweka wazi kuwa wanaenda kumkomboa mkulima.
Maige amesema mkataba huo ambao wameingia na KPMG umezingatia malengo yao ambayo yatawawezesha kufikia wakulima wengi, hivyo lengo la la wao kununua zaidi ya tani laki moja litatimia.
Amesema wameipa kazi hiyo kampuni ya KPMG kutokana na kuwa na uwezo mkubwa wa kuandaa mpango mkakati, taarifa za kodi, ukaguzi na ushauri, hivyo wana imani kuwa watafanya kazi katika muda ambao umepangwa, ili utekelezaji uanze haraka iwezekanavyo.
“Tumesaini mkataba huu na KPMG tukiamini kwamba tunaenda kupata mpango mkakati ambao unaenda kutufanya kuwa taasisi ya serikali ambayo itateka biashara ya ununuzi wa mazao, hivyo wakulima watanufaika kwa haraka.
Sisi tunawataka wakulima nchini kulima kwa wingi mazao ambayo tunahitaji kwani mnunuzi wa uhakika yupo,”amesema.
Kaimu Mkurugenzi huyo amesema CPB inatarajia kununua mazao kama shayiri, mpunga, soya, muhogo, ulezi, mahindi, uwele, mtama na mengine.
Aidha, Maige amesema CPB ina maghala katika Kanda tano za Arusha, Dodoma, Manyara, Iringa na Mwanza, hivyo kuwataka wakulima kuyatumia kwa ufanisi.
Amesema pamoja na changamoto zilizopo kwenye sekta ya kilimo, watahakikisha mpango mkakati mpya unaoanza 2023 hadi 2028 unaenda kumkomboa mkulima.
Kaimu mkurugenzi huyo, amesema kwa sasa wanauza mazao katika nchi zote za Afrika Mashariki na kwamba lengo ni kutanua wigo wa masoko.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa KPMG, Adolf Boya amesema mpango mkakati wanaoenda kutengeneza utaenda kutoa tafsiri sahihi ya dira ya maendeleo ya taifa.
Boya amesema wana uzoefu wa muda mrefu wa kuandaa mipango mikakati hivyo matumaini yao ni kufanya vizuri, ili CPB iweze kufikia malengo yake.
“Tumepewa muda wa miezi mitatu kukamilisha mpango mkakati huu wa CPB napenda kuahidi kuwa tutafanya katika ubora ambao unahitajika,” amesema.
Mwisho