Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt Venance Mwasse akizungumza na waandishi wa habari( hawapo pichani) kuhusu Mkutano wa Wachimbaji wadogo wa Madini utakaofanyika Jijini Dar es salaam April 5 hadi April 6 mwaka huu.
……………………….
Na Mwandishi Wetu
Imeelezwa kuwa Wachimbaji wadogo wa madini wanakumbwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa masoko ya uhakika pamoja na kukosa mitaji,hivyo Shirika la Madini la Taifa(STAMICO)limeandaa mkutano wa siku mbili kujadili changamoto hizo.
Hayo ameyasema April 4.2023 Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Dkt Evance Mwasse wakati akizungumza na waandishi wa habari nakubainisha kwamba Mgeni rasmi wa mkutano huo unaofanyika Aprili 5 na Aprili 6, 2023, anatarajiwa kuwa Waziri wa Madini Dotto Biteko.
Amesema kwamba mkutano huo utafanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere( JNICC) Dar es salaam nakwamba utawakutanisha wadau mbalimbali ikiwemo wachimbaji wa madini ya malighafi za viwandani,wamiliki wa viwanda ,pamoja na taasisi za kifedha(Bank) ili kujadili changamoto zinazowakumba wachimbaji hao pamoja na watu wenye viwanda ili kujua kwanini hawatumii malighafi za hapa nchini nakuweza kuchukua hatua.
Amendelea kusema kuwa mkutano huo unatarajiwa kuwakutanisha wachimbaji wadogo wa madini kutoka mikoa mbalimbali ,nakwamba mkutano huo una shabaha ya kuvifanya viwanda vifanye kazi kwa ufanisi ili kuzalisha bidhaa za bei nafuu na kuweza pia kushindana na soko la dunia.
” Wenye viwanda njooni ili mtoe changamoto zenu tufahamu nini hasahasa kinawakwamisha kutumia malighafi za hapa nchini,hii itatusaidia sisi kama shirika la Madini la Taifa kuchukua hatua za kuondoa changamoto hizo na kukuza sekta ya viwanda kama serikali ilivyoweka agenda ya kuhakikisha kuwepo kwa uchumi utokanao na viwanda” amesema Dkt Mwasse.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirikisho la Wenye Viwanda Nchini( Cti) Leodigar Tenga amesisitiza watu wenye viwanda kujitokeza kwa wingi ili kujadili kwa pamoja changamoto zinazowakabili ili waweze kutumia malighafi za viwandani zilizopo hapa nchini.
“Napenda nisisitize kwamba nchi yetu inataka ijenge uchumi wake kutokana na viwanda,tuna Madini yetu nchini ,tuna wajibu sisi kama Cti kuhamasisha watu wenye viwanda kutumia malighafi tulizonazo hapa nchini kwani wenye viwanda wanataka kuwepo na upatikanaji wa malighafi kwa wingi pamoja na ubora” amesema Tenga
Nae Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Madini Wadogo Mkoa wa Dar es salaam na Pwani ( DACOREMA) Josephat Mkombachepa pamoja na Katibu Mkuu wa Chama cha Wanawake Wachimba Madini Tanzania( TAWOMA) Salma Ernest wameishukuru serikali kupitia STAMICO kwa kuandaa mkutano huo kwani utawasaidia kuondoa changamoto zinazowakabili.
Mkutano huo pia utazishirikisha taasisi za udhibiti ikiwemo Mamlaka ya Mapato (TRA), Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira( NEMC), Tume ya Madini inayosimamia masuala ya leseni kwa wachimbaji wa madini pamoja na Maabara za Kupima Ubora wa Madini.