………………………….
Na Sixmund Begashe
Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Idara ya Mambo ya Kale imeanza mkakati maalum wa kuainisha, kuhifadhi na kuyatangaza maeneo ya kihistoria yanayopatikana katika Jiji la Dodoma kwa lengo la kulifanya Jiji hilo kuwa na vivutio vya kitalii vya kila aina kama ilivyo katika Majiji mengine Duniani
Hatua hiyo inakuja kufuatia kauli aliyoitoa siku chache zilizopita, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Mohammed Mchengerwa kuwa Tanzania imebariki kuwa na vivutio vya utalii vya kila aina mbali na wanyamapori na kama kila Mtumishi atawajibika ipasavyo idadi ya watalii ifikapo mwaka 2025 itaongezeka maradufu.
Kauli hiyo imemsukuma Mkurugenzi wa Idara ya Mambo Kale, Dkt.Christowaja Ntandu kutembelea maeneo ya Kihistoria yaliyopo Jijini hapo kama sehemu ya kufanikisha azma hiyo
Akizungumza mara baada ya kutembelea Makaburi ya Wahanga wa Vita vya Kwanza na vya Pili vya Dunia, Eneo la mnara wa Uhuru, Mnara wa Mashujaa wa Tanzania, Nyerere square na Hoteli ya Dodoma, Dkt.Ntandu amesema ziara hiyo ni mkakati maalum wa kushirikiana Wadau wa Utalii katika Jiji hilo kwa lengo la kuongeza mazao mapya ya Utalii hususan utalii wa Malikake kwenye maeneo mbalimbali nchini kuanzia ngazi ya kata mpaka Mkoa
Maeneo mengine aliyotembelea ni pamoja na eneo Kikuyu ambalo lina asili ya jina la Dodoma, Mti aina ya Mkuyu uliopo katika eneo la Chuo Kikuu cha St. John ambao ulitumika kunyongea wahalifu wakati wa Utawala wa Wajerumani
Akizungumzia Hoteli ya Dodoma ambayo licha ya kujengwa mwaka 1901 lakini bado ipo kwenye hali nzuri, Dkt.Ntandu amesema sehemu ya jengo hilo ikiwemo vyumba vya kulala wageni na baadhi ya vifaa vikiwemo meza na viti bado vinaendelea kutumika kutokana na uimara wake.
Kwa upande wake, Meneja wa Hoteli hiyo, Wellington Malea amesema kuwa wataendelea kuhifadhi hoteli hiyo ili iendelee kuwa kivutio kwa wageni kutoka ndani na nje ya nchi hususani Watalii kutoka Nchi ya Ujerumani kwa kuwa hoteli hiyo ilijengwa kipindi cha utawala wa Wajerumani wakati wakijenga Reli ya kati.
Katika ziara hiyo Mkurugenzi Christowaja Ntandu aliongozana na timu ya watalaamu wake wa Malikale, Afisa Utamaduni na Afisa Utalii wa Jiji la Dodoma.