Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimkabidhi mshindi wa kwanza wa kuhifadhi Juzuu (30) upande wa wavulana, Suleiman Omar Ally, Pikipiki, baada ya kuibuka mshindi wa pili wa mashindano ya kitaifa ya kuhifadhi Quran Tukufu yaliyoandaliwa na Taasisi ya Asha Sururu yaliyofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Jijini Dar es Salaam Aprili 02, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Mke wa Waziri Mkuu Mary Majaliwa akimkabidhi mshindi wa kwanza wa kuhifadhi Juzuu (30) upande wa wanawake, Asma Rubea Salehe, namba ya usajili ya pikipiki ya kubebea mizigo, baada ya kuibuka mshindi wa kwanza wa mashindano ya kitaifa ya kuhifadhi Quran Tukufu yaliyofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Jijini Dar es Salaam Aprili 02, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Mke wa Waziri Mkuu Mary Majaliwa akimkabidhi mshindi wa pikipiki wa kuhifadhi Juzuu (30) upande wa wanawake, Rabia Abdalah Qassim, Pikipiki, baada ya kuibuka mshindi wa pili wa mashindano ya kitaifa ya kuhifadhi Quran Tukufu yaliyoandaliwa na Taasisi ya Asha Sururu yaliyofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Jijini Dar es Salaam Aprili 02, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza waumini na viongozi wa dini ya Kiislam wakati alipomuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mashindano ya kitaifa ya kuhifadhi Quran Tukufu yaliyoandaliwa na Taasisi ya Asha Sururu yaliyofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Jijini Dar es Salaam Aprili 02, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir Bin Ally Mbwana akizungumza wakati wa mashindano ya kitaifa ya kuhifadhi Quran Tukufu yaliyoandaliwa na Taasisi ya Asha Sururu yaliyofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Jijini Dar es Salaam Aprili 02, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa dini kila wanapopata nafasi kwenye mimbari wakemee kuhusu ukatili wa kijinsia pamoja na wale wanaoenda kinyume na maadili na desturi za Kitanzania.
“Nitoe rai kwa viongozi wetu wa dini muendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kulinda mila, desturi na tamaduni za Kitanzania hususan katika kipindi hiki tunachokabiliwa na wimbi kubwa la mmomonyoko wa maadili,” amesema.
Ametoa wito huo leo (Jumapili, Aprili 2, 2023) wakati akizungumza na viongozi na waumini waliohudhuria mashindano ya kitaifa ya kuhifadhi Quran tukufu yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam. Mashindano hayo yaliandaliwa na taasisi ya Aisha Sururu Foundation (ASF).
“Sasa hivi Tanzania inakabiliwa na tatizo la mmomonyoko wa maadili na pia kumeibuka wimbi la vitendo vingine ambavyo vinakwenda kinyume kabisa na dini zetu pamoja na mila, desturi na tamaduni za kitanzania. Ninampongeza sana Dkt. Aboubakar bin Zubeir, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania kwa kulisimamia kidete suala hili ikiwa ni pamoja na kutoa maelekezo mahsusi kwa viongozi wote wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania kulikemea na kutolifumbia macho.”
Amesema licha ya kukithiri kwa vitendo hivyo vya mmomonyoko wa maadili, Waislamu wanajivunia uwepo wa Quran tukufu ambayo katika sura ya 33 aya ya 21 (Quran 33:21) wanakumbushwa kwamba wanacho kiigizo chema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu. “Kwa lugha nyingine Quran inapaswa kuwa chanzo cha kutegemewa cha mafunzo sahihi ya tabia njema, utii na kuheshimu mamlaka zilizopo,” amesisitiza.
“Tunapowahifadhisha Quran vijana wetu, tuhakikishe jambo hilo jema linakwenda sambamba na ujenzi wa misingi imara ya malezi itakayowafanya wawe raia wema, waadilifu na wazalendo kwa nchi yao. Tukiwa wazazi, walezi na walimu wa Quran, nitoe rai kwamba tunapotoka hapa hebu tujiulize ni kwa kiasi gani tunaizingatia hii Quran tukufu katika mwenendo mzima wa maisha yetu ya kila siku.”
Waziri Mkuu amesema kwa kufanya hivyo watakuwa wanamsaidia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye mara zote amekuwa akiguswa na suala zima la maadili hususan kwa vijana. “Pia tutamsaidia Mheshimiwa Rais kupata wasaidizi wacha Mungu na waadilifu katika kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wananchi.”
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaomba waumini hao waendelee kuiombea amani Tanzania kwani ikipotea mikusanyiko kama hiyo haitoweza kufanyika. Amesema Quran sura ya pili aya ya 126 (Quran 2:126) inawakumbusha umuhimu wa kuiombea nchi amani kupitia dua ya Nabii Ibrahimu alipouombea mji wake na wakazi wake amani na neema.
“Nasi tuendelee kuiombea nchi yetu na viongozi wake ili waendelee kuliongoza vema Taifa letu ikiwa ni pamoja na kujenga umoja na mshikamano, kudumisha amani na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii,” amesisitiza.
Mapema, Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Dkt. Aboubakar bin Zubeir alimpongeza Mwenyekiti wa taasisi ya ASF, Bi. Aisha Sururu kwa kuandaa mashindano hayo kwa miaka 22 na akamuelezea kwamba ni mwanamke pekee Tanzania na Afrika Mashariki ambaye anafanya kazi hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya Amana ambao ni wadhamini wakuu wa mashindano hayo, Bw. Aboubakar Athuman Ally alisema kwa mwaka huu wametenga sh. bilioni 40 kwa ajili ya uwezeshaji wa vikundi na wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa.
Akisoma risala ya ASF, Bi. Zainab Matitu Vulu alisema washiriki wa mashindano hayo wanatoka maeneo tofauti nchini ambao jumla yao walikuwa 600 kutoka mikoa 20 ya Tanzania bara na visiwani na baada ya mchujo waliofanikiwa kuingia fainali ni 77.
Aliyataja baadhi ya majukumu yao ni kuwaunganisha vijana wa shule za sekondari na vyuo vikuu, kutoa ufadhili kwa baadhi ya vijana, kuwafundisha stadi za maisha na kuwasaidia wajane.
Alisema wana kiwanja walichonunua ambacho kipo Kiparang’anda wilayani Mkuranga, lakini wanahitaji fedha za kujenga chuo cha kuwafundisha vijana stadi za maisha na kuwahifadhisha Quran tukufu