Na Dotto Mwaibale, Singida
MKOA wa Singida umeendelea kujidhatiti na kuongeza ufanisi
katika upatikanaji wa huduma bora za afya kwa kutekeleza afua mbalimbali ikiwa
ni pamoja na kutumia mfumo wa Mshitiri kwa bidhaa za afya zinazokosekana Bohari
ya Dawa (MSD).
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba wakati
akifungua mafunzo ya wawezeshaji wa Mfumo Mshitiri kutoka Halmashauri Saba za
mkoa huo ambazo ni Itigi, Iramba, Singida Manispaa, Ikungi, Manyoni, Singida DC
na Mkalama.
“Kutokana na changamoto na kuibuka kwa hoja mbalimbali za ununuzi wa bidhaa
za afya vituoni, Ofisi ya Rais – TAMISEMI
ilitoa waraka namba moja wa mwaka 2018 ambao ulielekeza matumizi ya washitiri
teule wa mikoa katika ununuzi wa bidhaa za afya pale vituo vinapokosa bidhaa
kutoka MSD,” alisema.
Serukamba alisema kuwa uwapo wa mfumo huo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM), kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kama
ilivyoainishwa katika sura ya Tatu, sehemu ya 81 (i) na (aa).
Alibainisha kuwa upatikanaji dawa na vipimo vya kitabibu kwa uhakika katika
kituo cha huduma za afya kwa kiasi kikubwa unaakisi ubora wa huduma zitolewazo
na mahali husika.Hivyo, alitoa mwito kwa washiriki kuzingatia utekelezaji wa
mwongozo wa mfumo huo ili waweze kuusimamia kikamilifu kwa ajili ya kuleta
matokeo chanya yanayolenga kuongeza upatikanaji wa bidhaa za afya kwenye vituo
vya kutolea huduma hizo.
Katika hatua nyingine, Mwezeshaji wa kitaifa kutoka Wizara ya TAMISEMI,
Emmanuel Mayunga, alisema semina hiyo inalenga kuwajengea uwezo washiriki ili
wanapomaliza waweze kusimamia vema Mfumo huo kulingana na mwongozo na sheria za
nchi
Mfamasia Elikana Lubango, alisema
mfumo Mshitiri ulianzishwa kwa mujibu washeria za ununuzi wa umma pamoja na
mpango mkakati wa kisekta ili kutatua changamoto za upatikanaji wa huduma bora
za afya nchini.Alisema Mfumo huo unasaidia wakati bidhaa za afya zinapohitajika
kwa dharura kupatikana mara moja tofauti na ilivyokuwa siku za nyuma.