Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Johari Samizi amesema miradi mbalimbali ya maendeleo yenye jumla ya fedha zaidi ya Bilion 13 imetekelezwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Disemba 2022 ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya CCM.
Ameyasema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi CCM ya Mwaka 2020 hadi 2025 kipindi cha Julai hadi Disemba Mwaka 2022 kwenye mkutano ambao umefayika katika ukumbi wa ofisi za CCM Wilaya ya Shinyanga mjini na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama pamoja na viongozi wa serikali wakiwemo wakuu wa idara katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.
DC Samizi amesema pato la wastani la mkazi wa Manispaa ya Shinyanga kwa Mwaka 2021 ni (zaidi ya Milioni moja) shilingi 1,861,770 kwa Mwaka.
Amesema Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga katika utekelezaji wa ilani ya CCM imetekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye sekta mbalimbali ikiwemo sekta za Elimu, Afya, ujenzi na maendeleo ya jamii, barabara na maji na kwamba miradi hiyo ina thamani ya jumla Tshs Bilioni 13,804966,547 katika Manispaa ya Shinyanga.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Johari Samizi amefafanua zaidi kuwa miradi hiyo ilihusisha ujenzi wa mashule, maeneo ya kutolea huduma za afya kama kituo cha afya na zahanati, majengo ya ofisi, kituo cha mabasi, mikopo kwa vikundi, barabara, miundombinu ya maji pamoja na sekta zingine.
Ametaja baadhi ya kata za Manispaa ya Shinyanga zilizofikiwa na miradi hiyo kuwa ni pamoja na kata ya Kambarage, Ngokolo, Ndembezi, Old Shinyanga, Ndala na kata ya Chamaguha.
Amesema Serikali katika kipindi hicho ilitoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo iliagiza kujenga na kuimarisha vituo vya kutolea huduma za afya ili viweze kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi hadi kufikia Mwaka 2025 ambapo serikali itaongeza vituo vya kutolea huduma za afya kwa asilimia 20 ya vituo.
Mhe. Samizi ameelezea zaidi maagizo mengine ya serikali kuwa ni pamoja na kuwezesha vijana kushiriki katika shughuli za ujasiriamali ikiwemo kuwapa mafunzo na kuwaunganisha na kuwawezesha mikopo ya fedha kwa vikundi, ukarabati wa miundombinu ya elimu pamoja na kuhifadhi na kuendeleza mazingira ya shule ikiwemo shule mpya ya mtaa wa Azimio katika kata ya Lubaga, ujenzi wa choo sekondari Kizumbi, ujenzi wa miundombinu shule ya wasichana Butengwa kata ya Ndembezi.
Amesema maagizo mengine ya serikali ni kuongeza ajira, kuboresha kasi ya utekelezaji awamu ya tatu ya TASAF ili kuwafikia wananchi maskini katika vijiji, mitaa yote kwa kutekeleza miradi ya kutoa ajira za muda ili kukuza uchumi wa kaya na kuendeleza rasilimali watu lakini pia amesema pamoja na kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji na usafi wa mazingira vijiji kutoka asilimia 63 hadi asilimia 85 ifikapo Mwaka 2025.
Aidha Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Johari Samizi katika taarifa yake ameelezea shughuli mbalimbali zinazoendelea kufanyika katika Manispaa ya Shinyanga.
“Manispaa ya Shinyanga ni miongoni mwa Halmashauri mbili zinazounda Wilaya ya Shinyanga Halmashauri hii inapakana na Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga upande wa Kaskazini Magharibi na Kusini Magharibi, na Kishapu kwa upande wa Mashariki na Kusini Mashariki”.
“Manispaa ina eneo la kilometa za mraba 548 ambapo kati ya eneo hilo, eneo la katikati ya mji lina kilometa za mraba 25 na eneo mchanganyiko na vijiji ni kilometa za mraba 523 shughuli kuu za kiuchumi ni kilimo na ufugaji, viwanda na Biashara na shughuli za maofisini”.amesema DC Samizi
“Kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi iliyofanyika Nchi nzima Mwaka 2012 Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga ilikuwa na jumla ya watu 161,391 ambapo kwa sasa kwa mujibu wa mamlaka ya takwimu Tanzania (NBS) kwa Mwaka 2020 Manispaa inakadiriwa kuwa na idadi ya watu wapatao 201,797 ambapo wanaume ni 98,289 na wanawake ni 103,508”.
“Kiutawala Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga ina tarafa tatu (3) kata kumi na saba (17), vijiji kumi na saba (17) mitaa 55 na vitongoji 84 katika kila ngazi kuna watendaji na viongozi thabiti waliochaguliwa na wananchi”.amesema DC Samizi
“Hali ya usalama ni shwari ukiacha matukio ya hapo na pale yanayoripotiwa na jeshi la polisi Manispaa imekuwa ikijitahidi kuwa mstari wa mbele katika kupiga vita vitendo vyote vya ukatili, ubaguzi na unyanyapaa kwa makundi yote”.
“Shughuli kuu za kiuchumi kwa Manispaa ya Shinyanga ni kilimo, ufugaji, biashara ajira za maofisini na shughuli za viwandani, asilimia 70 ya wakazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga hujishughulisha na kilimo na ufugaji mazao makuu ya chakula ni mahindi, mpunga, mtama, uwele, muhogo, viazi vitamu, dengu, choroko na karanga mazao ya biashara ni Pamba na Alizeti”.amesema DC Samizi
Wajumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Wilaya ya Shinyanga mjini wameipokea taarifa ya utekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi CCM ya Mwaka 2022/2023 katika kipindi cha Julai hadi Disemba Mwaka 2022.
Katika mkutano huo wajumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Wilaya ya Shinyanga mjini wameipongeza serikali kwa kuendelea kutekeleza ilani ya chama hicho huku wakimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Aidha wajumbe wa mkutano huo wamepata nafasi ya kutoa ushauri, maoni na kuuliza maswali mbalimbali juu ya changamoto zinazowakabili wananchi ambapo wataalam kutoa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga wamejibu maswali hayo huku Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Johari Samizi akipokea na kuahidi kwenda kushughulikia kero za wananchi.