Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (kushoto) akizungumza na wadau wa sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo katika mkutano wa majadiliano kati ya Wizara na wadau wa sekta binafsi uliofanyika mapema hii leo jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akizungumza na wadau wa sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo (hawapo pichani)wakati wa mkutano wa majadiliano kati ya Wizara na wadau wa sekta binafsi uliofanyika mapema hii leo jijini Dar es Salaam.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Dkt. Godwill Wanga akizungumza na wadau wa sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo (hawapo pichani) wakati wa mkutano wa majadiliano kati ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na wadau wa sekta binafsi uliofanyika mapema hii leo jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wadau wa sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo wakimsikiliza Mgeni rasmi Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (hayupo pichani) wakati wa mkutano wa majadiliano kati ya Wizara na wadau wa sekta binafsi uliofanyika mapema hii leo jijini Dar es Salaam.
…………………..
Serikali kupitia wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imeeleza mikakati mbalimbali na dhamira ya serikali ya awamu ya sita ya kutatua changamoto zinazozikabili sekta ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na wadau wa sekta hizo.
Akizungumza na wadau wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, katika mkutano wa majadiliano, Waziri mwenye dhamana hiyo Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema kuwa lengo la wizara ni kuhakikisha sekta hizo zinakuwa kwa kasi kwani wizara imechukua hatua ya kuandaa Mkakati wa Maendeleo wa michezo na kuendelea kufanya mapitio.
“Serikali kupitia wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuandaa mkakati wa maendeleo ya michezo na kuendelea kuafanya mapitio ya sera, sheria zinazosimamia sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo ili kupunguza changamoto zinazokabili sekta hizi”, alisema Dkt. Chana.
Dkt. Chana ameongeza kuwa ukuaji na maendeleo makubwa ya sekta hizi hayatokani na juhudi za Serikali peke yake bali unachangiwa pia na uwekezaji mkubwa unaofanya na sekta binafsi.“
Sekta binafsi imekuwa na mchango mkubwa katika ujenzi wa miundombinu ya michezo, ufadhili wa timu za mpira wa miguu kwa wanaume na wanawake, ufadhili wa ligi kuu ya Tanzania pamoja na uendelezaji wa vipaji vya sanaa na Utamaduni”, alisema Dkt. Chana.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara la Taifa (TNBC), Dkt. Godwill Wanga amesema kuwa lengo la mikutano hii ni kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan la kila taasisi na idara zake kukutana na wadau wake kwa lengo la kujua changamoto zinazowakabili.“
Mkutano huu ni utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais la kila taasisi na idara kukutana na wadau wake kwa lengo la kubaini changamoto wanazokutana nazo ili serikali iweze kutafutia ufumbuzi kwani kwa kufanya hivyo kutaweza kuongeza mapato kwa nchi”, alisema Dkt. Wanga.
Mkutano huu wa majadiliano ya kisekta kati ya wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na wadau wa sekta binafsi una lengo la kuboresha huduma zinazotolewa na sekta za utamaduni, sanaa na michezo kwani sekta hizi zina nguvu kubwa ya ushawishi, uhamasishaji na ustawishaji wa jamii na maendeleo ya nchi kupitia ajira.
Mwisho..