Mwandishi wa makala haya Albano Midelo akiwa amekaa kwenye gogo lililopo eneo la Matchedje nchini Msumbiji gogo hilo mwaka 1968 walikalia Rais Julius Nyerere wa Tanzania,Rais Edward Mondlane wa Msumbiji na Mkuu wa Majeshi alikuwa Samora Machel ambao walikaa kwenye gogo hilo kwa siku tano wakijadili namna ya kuikomboa nchi ya Msumbiji toka kwa wareno.Gogo hilo ambalo limehifadhiwa hadi leo ni kivutio adimu cha utalii
Alfonso Kaidavid ni Mhifadhi kwenye makumbusho ya Taifa ya Msumbiji yaliyopo Matchedje Jimbo la Niassa, anasema serikali iliamua kuanzisha makumbusho katika eneo hilo kutokana na kufanyika mkutano wa pili mwaka 1968 uliosababisha nchi hiyo kupata uhuru wake mwaka 1975
picha hii ilipigwa katika kijiji cha Muhukuru wilayani Songea mkoani Ruvuma,kijiji hicho kipo mpakani mwa nchi ya Tanzania na Msumbiji,ilipigwa katika harakati za ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika pichani waliopo ni Mwl.Julius Nyerere Rais wa zamani wa Tanzania,Samora Machel wa Nsunbiji na Keneth Kaunda wa Zambia
………………
NCHI ya Tanzania wakati huo ikiwa chini ya uongozi wa Rais wa Awamu ya Kwanza Hayati Mwl.Julius Nyerere ilishiriki kikamilifu kwenye harakati za ukombozi kusini mwa Afrika.
Nchi ya Msumbiji ni miongoni mwa nchi ambazo hazitaisahau Tanzania ilivyotoa mchango wake hadi kusababisha nchi hiyo kupata uhuru wake toka kwa wareno mwaka 1975.
Alfonso Kaidavid ni Mhifadhi kwenye makumbusho ya Taifa ya Msumbiji yaliyopo Matchedje Jimbo la Niassa, anasema serikali ya Msumbiji imeamua kuanzisha makumbusho katika eneo hilo kutokana na kufanyika mkutano wa pili mwaka 1968 uliosababisha nchi hiyo kupata uhuru wake.
Anasema mkutano wa kwanza wa harakati za kuikomboa Msumbiji ulifanyika jijini Dar es salaam nchini Tanzania mwaka 1962 ukiongozwa na Rais Julius Nyerere wa Tanzania na viongozi waandamizi wa FRELIMO nchini Msumbiji ambao ni Edwardo Mondlane na Samora Machel..
Mhifadhi Kaidavid anasema Mkutano wa pili ulifanyika kwa siku tano katika eneo la Matchedje kuanzia Julai 20 hadi 25 mwaka 1968 na kwamba mkutano huo ulioongozwa viongozi waandamizi wakiwemo Rais Julius Nyerere wa Tanzania,Edwardo Mondlane na Samora Machel wa Msumbiji.
“Makumbusho haya tumeanzisha ili wanamsumbiji,watanzania na wageni wengine kutoka nchi mbalimbali waweze kujua ni namna gani nchi ya Msumbiji ilipambana katika kuikomboa nchi toka kwa wakoloni wareno ambao walitutawala kwa miaka mingi’’,anasisitiza Kaidavidi.Anamtaja kiongozi wa FRELIMO hayati Edward Mondlane kwa kushirikiana na Samora Machel walipata mafunzo mbalimbali nje ya nchi ya Msumbiji namna ya kumfukuza mkoloni ili kuiacha Msumbiji huru.
Mhifadhi huyo anasema kabla ya kuamua kumwaga damu viongozi hao walijaribu kuzungumza na wareno ili wakubali kwa hiyari kutoa uhuru wa Msumbiji,hata hivyo ilishindikana ndipo waliamua kutumia njia ya bunduki.
Historia inaonesha kuwa wareno walifika nchini msumbiji mwaka 1498 na kwamba safari yao ilikuwa ni kwenda nchini India,hata hivyo waliamua kubaki Msumbiji,baada ya kubaini nchi hiyo ina utajiri mkubwa wa madini na meno ya tembo.
Akizungumzia vivutio vya utalii vilivyopo eneo hilo la kihistoria la Matchedje,Kaidavid anasema kwenye eneo hilo yamebakia masalia ya vibanda mbalimbali ambavyo viongozi wa kitaifa waliishi kwa siku tano kufanya mkutano wa pili mwaka 1968 uliozaa uhuru wa Msumbiji.
Moja ya vivutio kwenye eneo hilo ni uwepo wa gogo ambalo mwaka 1968 walikalia Rais Julius Nyerere wa Tanzania,Rais Edward Mondlane wa Msumbiji na Mkuu wa Majeshi alikuwa Samora Machel ambao walikaa kwenye gogo hilo kwa siku tano wakijadili namna ya kuikomboa nchi ya Msumbiji toka kwa wareno.
“Viongozi hao mwaka 1968 walijadili wakiwa wamekaa kwenye gogo hili ambalo hadi leo bado lipo likiwa vile vile bila kuoza,tumelihifadhi kama kumbukumbu muhimu kwenye harakati za ukombozi wa nchi ya Msumbiji’’,anasisitiza Mhifadhi huyo.Maeneo mengine ambayo ni kivutio kwenye eneo hilo ni uwepo wa kibanda ambacho alilala kwa siku tano Rais wa Msumbiji Edwardo Mondlane mwaka 1968,pia kuna kibanda ambacho alilala Mkuu wa Majeshi Samora Machel kwa siku tano na kibanda ambacho walilala waandishi wa habari kwa siku tano.Ukiachia harakati zilizoendelea nchini Msumbiji, eneo la Masonya lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma nchini Tanzania lina utajiri wa utalii wa malikale na utambulisho wa Taifa,ingawa bado halifahamiki na wengi.
Eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 100 lina vivutio adimu vya utalii wa malikale ikiwemo nyumba yenye namba A 10 ambayo walikuwa wanafikia na kuishi Marais Hayati Julius Nyerere wa Tanzania na Hayati Samaro Machel wa Msumbiji kuanzia 1966 wakati wa harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika.
Mhifadhi wa Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Bartazar Nyamusya anasema viongozi hao pia wakiwa katika nyumba hiyo,walitumia jengo dogo maalum lililopo jirani ya nyumba hiyo kama chumba cha mawasiliano yote na nchi zilizokuwa katika harakati za ukombozi kusini mwa Afrika.
Kutoka nyumba ya viongozi hao hadi jengo dogo la mawasiliano,lilijengwa handaki la chini kwa chini ambalo lipo hadi sasa lililokuwa linatumiwa na viongozi hao wa Tanzania na Msumbiji.