Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na wananchi wa Majani ya Chai kata ya Maweni jijini Tanga alipoenda kuwatembelea kwa lengo la kuwashukuru kwa jitihada zao za kukiunga mkono Chuo cha Utumishi wa Umma kupata hati ya kumiliki kiwanja kwa ajili ya kujenga kampasi ya chuo hicho jijini humo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa na viongozi pamoja na wananchi wa Majani ya Chai Kata ya Maweni jijini Tanga wakati akiwasili eneo ambao Chuo cha Utumishi wa Umma kimepata kiwanja kwa ajili ya kujenga kampasi yake jijini Tanga.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akioneshwa ramani ya kiwanja cha Chuo cha Utumishi wa Umma na Kamishna wa Ardhi jijini Tanga alipowasili eneo ambalo chuo hicho kitajenga kampasi yake jijini humo.
Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mhe. Hashim Mgandilwa akizungumza na wananchi wa Majani ya Chai kata ya Maweni jijini Tanga kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kuzungumza na wananchi hao.
Diwani wa Kata ya Maweni, Mhe. Joseph Kolivasi akimshukuru Mhe. Jenista Mhagama kwa kuwatembelea wananchi wa kata yake wakati alipoenda kulitazama eneo ambalo Chuo cha Utumishi wa Umma kitajenga kampasi yake jijini Tanga.
……………………………..
Na. James K. Mwanamyoto-Tanga
Tarehe 29 Machi, 2023
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Mhe. Jenista Mhagama amewapongeza wakazi wa Majani ya Chai Kata ya
Maweni jijini Tanga kwa kukipambania Chuo cha Utumishi wa Umma (TPSC)
kupata eneo la kujenga kampasi itakayokuwa na manufaa ya vizazi vyao, kwa
wakazi wa mkoa huo na Watanzania wote watakaopata fursa ya kupata elimu
katika kampasi hiyo pindi ujenzi wake utakapokamilika.
Mhe. Jenista ametoa pongezi hizo wakati akizungumza na wananchi wa Majani
ya Chai Kata ya Maweni jijini Tanga alipoenda kuwatembelea kwa lengo la
kuwashukuru kwa kukiunga mkono Chuo cha Utumishi wa Umma kupata umiliki
wa kiwanja ili kujenga kampasi jijini humo.
Mhe. Jenista amesema kuwa, wakazi wa Majani ya Chai jijini Tanga wametoa
somo kwa Watanzania kwani maeneo mengine, Serikali ikitaka kujenga
miundombinu endelevu kwenye eneo lenye mgogoro wa ardhi mara nyingi
wananchi wanakuwa upande wa wanaodai kumiliki viwanja licha ya kushindwa
kuviendeleza, hivyo wananchi wa Majani ya Chai wanapaswa kuwa mfano wa
kuigwa kwa kupambania ujenzi wa chuo kwa manufaa ya taifa.
“Nimefurahishwa sana na uamuzi wenu wa kulilinda na kulipambania eneo hili na
hatimaye Chuo cha Utumishi wa Umma kimepata kiwanja cha kujenga kampasi
na kuongeza kuwa, limekuwa ni somo tosha ya namna ya kuisaidia Serikali
kupata eneo la kujenga miundombinu yenye tija kwa Serikali na wananchi pia,”
Mhe. Jenista amesisitiza.
Mhe. Jenista amesema, changamoto iliyokuwepo ilikuwa ni upatikanaji wa eneo
la kujenga kampasi ya chuo jijini Tanga, hivyo amemshukuru Kamishna wa Ardhi
jijini Tanga kwa kutoa taarifa rasmi kuwa kiwanja hicho ni mali ya Chuo cha
Utumishi wa Umma mara baada ya kufanyika kwa mchakato wote wa kisheria
wa umilikishaji ardhi kwenye eneo lililokuwa na mgogoro.
“Tumejipanga kujenga kampasi yetu wenyewe kwani tunapanga jengo la
kuendesha shughuli za chuo ambalo linatugharimu shilingi milioni 84 kwa
mwaka, hivyo leo wananchi wa Majani ya Chai mmeokoa fedha hiyo ya Serikali
na kuiwezesha Serikali kutekeleza mpango wa kujenga uwezo wa rasilimali watu
iliyonayo kupitia mafunzo yatakayotolewa na kampasi hiyo kwa watumishi wa
umma,” Mhe. Jenista amefafanua.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mhe. Hashim Mgandilwa
amesema wananchi wa eneo hilo wametekeleza wajibu wao kwa kukipambania
Chuo cha Utumishi wa umma kupata eneo la kujenga kampasi jijini Tanga, hivyo
amewataka kuendelea kulilinda eneo hilo mpaka ujenzi utakapokamilika.
Naye, Diwani wa Kata ya Maweni, Mhe. Joseph Kolivasi amemshukuru Mhe.
Jenista kwa kuwatembelea wananchi wa kata yake na kuongeza kuwa,
anaamimi kuwa Kampasi ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanga itaanza
kujengwa mapema iwezekenavyo na si kujengwa katika eneo lingine kama
ambavyo wananchi wa eneo analolitawala wanavyotarajia.
Mmoja wa wakazi wa Kata ya Maweni, Mzee Abdallah Kilo amesema amefurahia
kitendo cha Chuo cha Utumishi wa Umma kupewa umiliki wa eneo hilo ili
kujenga kampasi kwa manufaa ya kizazi kijacho, kwani ndio jambo ambalo yeye
na wenzie wamekuwa wakilipambania kwa nguvu zao zote.
Kaimu Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma
Tanzania (TPSC) Dkt. Ernest Mabonesho amewashukuru wananchi wa eneo hilo
kwa kuunga mkono jitihada za chuo chake kupata kiwanja kwa ajili ya kujenga
kampasi jijini Tanga na kuongeza kuwa eneo hilo limepatikana kwa jitihada za
wananchi hao.
. Mabonesho amemshukuru Kamishna wa Ardhi kwa kukamilisha taratibu za
kisheria zilizokiwezesha chuo chake kumiliki kiwanja hicho kwa ajili ya ujenzi wa
Kampasi ya Tanga.
Sanjari na hilo, amemshukuru Mhe. Jenista Mhagama kwa uamuzi wake wa
kuwatembelea wananchi wa eneo hilo ili kuwashukuru kwa mchango wao katika
upatikanaji wa kiwanja hicho.
Chuo cha Utumishi wa Umma kimemilikishwa eneo la ekari 12 kwa ajili ya ujenzi
wa kampasi yake jijini Tanga, kampasi inayotarajiwa kutoa mchango wa kujenga
uwezo wa kiutendaji wa rasilimaliwatu ya taifa.