Na Catherine Mbena/Arusha
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Anderson Mutatembwa amelitaka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika Hifadhi za Taifa katika nyanja za kimataifa zaidi ili kutimiza adhma ya kufikisha watalii milioni tano na mapato fedha za kimarekani dolla bilioni sita ifikapo mwaka 2025.
Akizungumza na watumishi wa TANAPA Makao Makuu, Naibu Katibu Mkuu alisema “Mfumo wa utangazaji wa vivutio tulivyonavyo uzingatie zaidi kutangaza katika vyanja za kimataifa ili kuweza kuongeza idadi ya watalii kutoka tuliyonayo sasa na kufikia watalii milioni tano ifikapo 2025, Mhe. Rais Samia alishatufungulia njia kupitia filamu ya Royal Tour wakati ni sasa kwenda kimataifa”
Mutatembwa pia amepongeza juhudi zinazofanywa na TANAPA katika kulinda rasilimali zilizopo katika hifadhi hizo licha ya kuwa na maeneo makubwa ya kazi.
“Niwapongeze kwa kazi nzuri na kubwa mnayoifanya ya kupambana na ujangili lakini pia kutoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi jirani na umma kwa ujumla. Maeneo mliyonayo ni makubwa sana lakini mnapambana.” Alisema Naibu Katibu Mkuu.
Aidha, alisema kuwa lengo la kufika kwake uwandani ni pamoja na kupanua uelewa wa masuala ya uhifadhi ili kuweza kutoa maamuzi yenye tija na yanayotekelezeka na kusisitiza kuwa utatuzi wa changamoto zilizo ndani ya uwezo wa taasisi ufanyike kwa wakati.
Awali akiwasilisha taarifa ya shirika kwa Naibu Katibu Mkuu, Kamishna wa Uhifadhi, William Mwakilema alimweleza kuwa hali ya mandeleo ya miradi ya kimkakati ya kukuza utalii inaendelea vizuri ikiwemo miradi ya miundombinu ya malazi katika Hifadhi ya Taifa Burigi –Chato na Kisiwa cha Rubondo na pia miradi ya UVIKO 19 katika Hifadhi ya Taifa Serengeti, Tarangire, Kilimanjaro, Mkomazi, Saadani na Nyerere inayolenga kuboresha miundombinu ya malango ya kuingilia wageni, barabara, na viwanja vya ndege.