Mwenyekiti wa Usalama Barabarani Mkoa wa Mbeya ndugu Rajabu Buliku kwa
niaba ya wajumbe wa kamati ya usalama barabarani mkoani hapa, amekabidhi Gari
yenye thamani ya Tshs.Milioni 28 aina ya Toyota Harrier kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa
Mbeya ikiwa ni sehemu ya utekelezaji majukumu ya kamati.
ya makabidhiano imefanyika Machi 29, 2023 ofisi ya kamanda wa Polisi Mkoa
wa Mbeya na kuhudhuriwa na wajumbe wa kamati ya usalama barabarani ya Mkoa.
Akizungumza baada ya kukabidhi Gari hilo, Mwenyekiti wa kamati ya usalama
barabarani Mkoa wa Mbeya Ndugu Rajabu amesema kuwa, Kamati hiyo itafanya
kazi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kupunguza ajali ndani ya Mkoa wa Mbeya.
Aidha ameongeza kuwa, Gari waliyokabidhi itatumika katika kurahisisha utendaji kazi
za askari wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Mbeya.
Makabidhiano hayo yalitanguliwa na uzinduzi wa kamati mpya ya usalama
barabarani Mkoa wa Mbeya katika kikao rasmi kilichofanyika chini ya Uenyekiti wa
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya ACP Benjamin Kuzaga.
Akizindua kamati hiyo, Kamanda Kuzaga amesema kuwa, uzinduzi wa kamati hiyo ni
takwa la kisheria na ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya viongozi wakuu wa
nchi waliyoyatoa katika maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani
yaliyofanyika kitaifa Jijini Mwanza.
Aidha ameongeza kuwa kazi ya kamati hiyo ni pamoja na kushirikiana na Jeshi la
Polisi kuzuia na kudhibiti ajali, kutoa elimu na kuwezesha vitendea kazi ambavyo
vitarahisisha kazi ya askari wa kikosi cha usalama barabarani ikiwemo kufika
maeneo mbalimbali na kutoa elimu, kufanya doria barabara kuu na maeneo tete.
Pia ametoa shukurani za dhati kwa kamati hiyo kwa kukabidhi gari ambalo litakuwa
msaada mkubwa kwa askari hasa katika kutekeleza mikakati ya mkoa katika kuzuia
ajali.