……………………
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameeleza kuwa Wizara ya Madini na Wizara ya Maliasili na Utalii zitashirikiana kuandaa Miongozo ya Uchimbaji wa Madini katika Maeneo ya Hifadhi hususan maeneo ya TFS ili kuwezesha shughuli za uchimbaji zifanyike.
Dkt. Kiruswa amesema hayo Machi 25, 2023 wilaya ya Mlele Mkoani Katavi alipotembelea eneo lenye katazo la uchimbaji madini ya dhahabu katika msitu wa Mlele Hills Kanono.
Amesema kuwa, Serikali ipo kwenye hatua ya kuandaa miongozo na taratibu zitakazowezesha shughuli za uchimbaji katika maeneo ya hifadhi kutatuliwa ili kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na kwa Taifa.
“Rais wetu anataka wachimbaji wanufaike na rasilimali madini zilizopo nchini, hivyo utaratibu mzuri wa uchimbaji katika maeneo ya hifadhi unaandaliwa ili kurahisisha uchimbaji kwenye hifadhi kuwa wa tija nchini” amesisitiza Dkt. Kiruswa.
Aidha, Dkt. Kiruswa amewataka wachimbaji hao kuheshimu taratibu zilizoweka na TFS katika maeneo hayo ili kuepusha migogoro ya wachimbaji katika hifadhi, amewataka washirikiane na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ili uchimbaji usiendelee katika maeneo hayo ya hifadhi.
Naye, Kaimu Afisa Madini wa Mkoa wa Katavi Mhandisi Paul Veran amesisitiza kushirikiana na TFS pamoja na wachimbaji wadogo kuhakikisha anakagua mara kwa mara ili kujiridhisha hakuna shughuli za uchimbaji zinazofanyika kinyemela katika eneo hilo.
Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Mlele Majid Mwanga amemhakikishia Dkt. Kiruswa kuwa, maelekezo yote aliyoyatoa ya kusimamisha shughuli za uchimbaji katika maeneo ya hifadhi yatazingatiwa hadi maelekezo yatakapotolewa.
Akizungumza katika kikao hicho, Simon Mdamila mchimbaji mwenye leseni katika eneo la hifadhi ameiomba Serikali ikamilishe mapema taratibu ili aweze kuendelea na shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu katika eneo hilo. Pia amemshukuru Naibu Waziri kuwatembelea na kuzungumza na wachimbaji kujua changamoto zinazowakabili.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Wataalam kutoka Wizara ya Madini, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Katavi na wawakilishi kutoka Wakala wa Misiti Tanzania (TFS).