Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipanda mti baada ya kukagua na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Shule ya Sekondari Njalu wilayani Itilima akiwa kwenye ziara ya Mkoa wa Simiyu, Machi 24, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa kwenye moja ya madarasa ya Shule ya Sekondari Njalu wakati alipokagua na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Shule hiyo wilayani Itilima akiwa kwenye ziara ya mkoa wa Simiyu, Machi 24, 2023. Kulia kwake ni Mbunge wa itilima, Silanga Njalu. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akitazama dawati wakati alipokagua na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Shule ya Sekondari Njalu wilayani Itilima akiwa kwenye ziara ya mkoa wa Simiyu, Machi 24, 2023. Kulia ni Mbunge wa Itilima, Silanga Njalu. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa ghala la kuhifadhia nafaka kwenye kijiji cha Ikindilo wilayani Itilima akiwa katika ziara ya Mkoa wa Simiyu, Machi 24, 2023. Wa nne kushoto ni Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde, wa tatu kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Dkt Yahya Nawanda, kulia ni Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi, Mhandisi Kundo Mathew na kushoto ni Mbunge wa Viti Maalum Esther Midimu.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi wakati alipowasili kwenye kijiji cha Ikindilo wilayani Itilima linapojengwa ghala la kuhifadhia nafaka, kukagua ujenzi huo na kuweka jiwe la msingi akiwa kwenye ziara ya mkoa wa Simiyu, Machi 24, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Wananchi wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipozungumza baada ya kukagua na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa ghala la kuhifadhia nafaka katika kijiji cha Ikindilo wilayani Itilima akiwa katika ziara ya mkoa wa Simiyu, Machi 24, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Ghala la kuhifadhia nafaka ambalo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alikagua ujenzi wake na kuweka jiwe la msingi akiwa katika ziara ya Mkoa wa Simiyu, Machi 24, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
…………………………..
* Wabunge wa Simiyu wammwagia sifa Rais Samia
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa shule ya sekondari ya Njalu katika kijiji cha Kimali, kata ya Nyamalapa, wilayani Itilima, mkoani Simiyu na kuagiza kwamba shule hiyo iwe ya mfano.
“Ujenzi wa shule hii usiishie kwenye madarasa na majengo ya utawala tu, bado inahitaji mabweni ya wavulana na wasichana, bwalo, viwanja vya michezo, nyumba za walimu na hapo baadaye tuwe na kidato cha tano na cha sita,” alisema.
Shule hiyo iliyojengwa kwa fedha za ndani za Halmashauri ya Itilima hadi sasa ina madarasa sita yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 45 kila moja.
Ametoa agizo hilo jana jioni (Ijumaa, Machi 24, 2023) wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Kimali kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya shule hiyo, mara baada ya kuikagua na kuweka jiwe la msingi.
Akitoa ufafanuzi kuhusu suala la umeme, Waziri Mkuu alisema wilaya hiyo imetengewa sh. bilioni 30 na kusisitiza kwamba mkakati wa Serikali wa kupeleka umeme vijijini uko palepale.
Mapema, Waziri Mkuu alizindua mradi wa ghala la kuhifadhi mazao ya chakula katika kijiji cha Ikindilo, wilayani Itilima ambao umelenga kudhibiti sumukuvu kwenye mazao ya chakula.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo mbele ya Waziri Mkuu, Meneja wa mradi huo, Eng. Mohamed Kombo alisema ujenzi wa ghala hilo na miundombinu yake ulianza Agosti 9, 2021 na kukamilika Februari 15, 2023. Mradi unafadhiliwa na GAFSP, Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) na Serikali Kuu.
“Lengo la mradi huu ni kusaidia kutoa elimu ya uhifadhi na kudhibiti sumukuvu kwenye mazao ya chakula ili kupunguza madhara yatokanayo na utumiaji wa mazao yaliyochafuliwa na kuvu inayosababisha sumukuvu,” alisema.
</Alisema ujenzi umekamilika kwa asilimia 100, na mkandarasi amekwishakabidhi mradi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima na ameanza kipindi cha uangalizi (defect liability period) cha mwaka mmoja.
Alisema Wizara ya Kilimo kupitia mradi wa TANIPAC ipo katika hatua za mwisho za ununuzi ya vifaa vya ghala na maabara ikiwemo chaga za kuhifadhia magunia, mashine ya kupima sumukuvu (Aflatoxin screen-kit), mashine ya kupima unyevu, komputa ya mezani na mizani. Vifaa hivyo vinatarajiwa kufikishwa kwenye mradi Mei, mwishoni.
Alisema mradi ulitengewa sh. milioni 990.5 na mkandarasi amekwishalipwa sh. milioni 850 sawa na asilimia 86 mpaka sasa. “Gharama halisi ya ujenzi itajulikana baada ya kufanya ukaguzi na malipo ya mwisho baada ya kipindi cha uangalizi kukamilika (Final Account).
Wakati huohuo, Wabunge wa mkoa wa Simiyu walipopewa nafasi kusalimia wananchi wa maeneo hayo, kwa nyakati tofauti, walimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwenye miradi ya elimu, afya, maji, barabara na umeme.
Walisema uwepo wa miradi hiyo umesaidia kusogeza huduma karibu na wananchi na mingine imechangia kuleta maendeleo ya haraka kwenye vijiji, kata na hata wilaya.