Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO) Stella Joel (wa nne kutoka kushoto) akizungumza katika mkutano uliohusu kongamano la fursa la Wanamuziki litakalofanyika kuanzia Mei 22 hadi 27, 2023 katika viwanja vya Makumbusho ya Taifa ya ElimuViumbe jijini Arusha.
……………………………..
Na Dotto Mwaibale, Arusha
UMOJA waWana muziki Tanzania (TAMUFO) kwa kushirikiana na Makumbusho ya
Taifa wameandaa kongamano la fursa litakalofanyika kuanzia Mei 22 hadi 26, 2023
katika viwanja vya Makumbusho ya Taifa ya ElimuViumbe jijini Arusha.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Arusha leo Machi
24, 2023, Katibu Mkuu wa TAMUFO, Stella Joel alisema kongamano hilo la siku
sita lenye kauli mbiu isemayo Twende na Muziki katika Maendeleo ya Taifa Letu
litawajumuisha wanamuziki wakongwe, vijana pamoja na wadau wa maendeleo na
jamii kwa ujumla.
“Kongamano hili ni la kihistoria ambalo halijawahi kufanyika hapa
nchini kabla ya uhuru na baada ya uhuru hivyo haitakiwi mtu kulikosa,”
alisema Joel.
Joel alisema muziki Umetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi ambapo alimtaja Mhasisi wa Taifa letu Mwalimu Julias
Kambarage Nyerere kuwa aliwatumia wanamuziki katika kuhamasisha maendeleo ya
Taifa wakiimba nyimbo zenye ujumbe wa kufundisha na kukemea maovu na kuwatetea
waafrika wenzetu kama Afrika Kusini,
Zimbabwe na maeneo mengine ya Afrika.
Alisema hata wakati wa Muungano Mwaka 1964 Nyimbo ziliimbwa kuhakikisha
unafana ambapo wanamuziki waliimba nyimbo za kuhamasisha uzalendo, nidhamu
kazini pia kukemea vitendo vya rushwa, uhujumu uchumi, walanguzi na wafujaji wa
mali ya umma.
“Ndugu zangu muziki una nguvu hata kwenye vitabu vya dini tunasoma
kwamba uliweza kuangusha ngome za Jerico hivyo kuna haja ya kuendelea
kuhuhamasisha kwa nguvu zetu zote
uendelee kutuletea maendeleo ya
Taifa letu n,” alisema Joel.
Alisema katika Kongamano hilo tayari wanamuziki kutoka sehemu mbalimbali
hapa nchini, vikundi vya bendi, waimbaji binafsi wameanza kujiandaa kwenda
jijini Arusha kushiriki kongamano hilo la kihistoria ambalo limesheheni fursa
lukuki kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo, Taasisi za kiserikali na za Kiraia ambao
watakuwepo kutoa elimu katika nyanja za Sanaa.
Joel alisema kupitia kongamano hilo wanamuziki watapata nafasi ya
kufahamiana na wenzao ambao watatoka nje ya nchi na kupata fursa ya kusikia
hotuba kutoka kwa viongozi wa Serikali
Aidha Joel alitumia nafasi hiyo kuwashukuru viongozi wa Wizara ya Utamaduni
Sanaa na Michezo ambao wanatoa
ushirikiano mkubwa kuhakikisha Kongamano hiloi linafanyika kwa kushirikiana na
BASATA na COSOTA ambao watakuwepo kwenye kongamano hilo.
Mkurugenzi wa Makumbusho ya Elimu Viumbe Arusha, Dk. Christina Ngerza,
alisema Makumbusho hiyo imejipanga
vizuri kutoa Elimu ya Uhifadhi wa Urithi wa Utamaduni na kuwa wanamuziki ni
watu muhimu katika kuhamasisha Maendeleo ya nchi hivyo Makumbusho itaendelea
kushirikiana na TAMUFO ili Kuwajengea uelewa Wanamuzi jinsi ya kuhifadhi urithi wa utamaduni
wetu katika nyanja mbalimbali.
Meneja Biashara Maendeleo wa Benki ya NBC Mkoa wa Arusha, Prince Moshi
akimwakilisha Meneja wa benki hiyo Mkoa wa Arusha alisema benki hiyo inaunga
mkono Juhudi hizo ambapo kupitia kongamano hilo watatoa fursa za Kibenki
kuhakikisha Muziki na Wanamuziki wanapata Bima ya Afya na Mikopo na Elimu za
Kibenki kwa maendeleo ya Tasinia hiyo.