Mama Janeth Magufuli, Mjane wa aliyekuwa Rais wa awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Hayati John Pombe Magufuli ametunukiwa Tuzo ya Heshima ya Kimataifa toleo la tatu, inayotolewa na taasisi ya Martha Tshisekedi Kasalu maarufu M. T. Kasalu, kutambua mchango wake kwa Taifa la Tanzania na kwa Hayati Rais Magufuli akiwa Rais wa Awamu ya Tano wakati akitekeleza majukumu yake Kitaifa na Kimataifa.
Aidha, Tuzo hii hutolewa kwa Wenza “spouses’ wa Viongozi Wakuu wa Nchi na watu Maarufu duniani kwa kutambua michango yao kwa Wenza wao, jamii na Taifa husika.
Tuzo hii ifahamikayo zaidi kama *M. T. Kasalu, Femme D’Honneur Trophee,* ilitolewa jana Ijumaa tarehe 24 Machi, 2023 katika hoteli ya Pullman jijini Kinshasa.
Waandaaji wa Tuzo hii ni Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Urithi ya Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo *DRC* wakishirikiana na Taasisi ya Lizadeel.
Kwa mwaka huu waliopokea tuzo hii ya M. T. Kasalu, toleo la 3 ni;
1. Mama Janeth MAGUFULI – Tanzania – mchango wake kwa Rais wa Awamu ya Tano unafahamika Afrika na duniani kote.
2. Mama Suzanne MUKAY – Congo Mke wa Daktari maarufu nchini DRC, wa magonjwa ya kina Mama na kansa, mumewe ameisaidia jamii kwenye nyanja hizo.
3. Mama Vivianne DALO – Mke wa Mchungaji Maarufu na anayeheshimika nchini DRC, Pastor Roland Dalo. Amesaidia jamii hasa wajane, yatima na vijana katika kujitegemea.
4. Mama Colette SENGHOR mke wa Rais wa kwanza wa Senegal, Mhe. Leopold Sedar Senghor , aliisaidia Senegal kupata Uhuru.
5. Mama Coretta KING mke wa Martin Luther King, USA. Mumewe alisaidia mengi ikiwemo kupinga ubaguzi wa rangi USA.