Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.
………………..
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekabidhi msaada wa kibinadamu kwa Serikali ya Malawi kwa ajili ya kuwasaidia wahanga wa kimbunga Freddy kilichosababisha mafuriko yaliyoikumba nchi hiyo Machi 13, 2023 na kusababisha madhara mbalimbali ikiwemo vifo vya zaidi ya watu 400.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga, amesema kuwa msaada huo umekabidhiwa kwa Rais wa Jamhuri ya Malawi, Mhe. Dkt. Lazarus Chakwer Machi 20, 2023 katika hafla fupi iliyofanyika katika Ikulu Jijini Lilongwe na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Malawi na Tanzania akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Mhe. Nancy Tembo na Balozi wa Tanzania nchini humo, Mhe. Humphrey Polepole.
Amesema kuwa msaada huo wa kibinadamu uliotolewa ni fedha taslim na vifaa mbalimbali wenye ya thamani ya Dola za Marekani Milioni Moja.
Amefafanua kuwa msaada huo pia unajumuisha chakula, vifaa vya kuokolea, vifaa vya kujihifadhi, Helikopta 2 za kijeshi zitakazotumika kupeleka misaada katika uokoaji pamoja na wanajeshi 100 watakaoshiriki kusambaza msaada huo; Mahema 50; Blanketi 6,000; Tani 1,000 za unga wa mahindi na fedha taslim kiasi cha Dola za Marekani 300,000.
“Rais wa Malawi, Mhe. Dkt. Lazarus Chakwera amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Wananchi wa Tanzania kwa msaada uliotolewa kwao na kueleza furaha yake kwamba msaada huo umewafikia kwa haraka na kwa wakati” amesema Balozi Kasiga
Msaada huo ni ishara ya undugu na mshikamano uliopo kati ya Tanzania na Malawi na kukumbusha kwamba hii si mara ya kwanza kwa Tanzania kuisiadia Malawi kwani iliwahi kufanya hivyo mwaka 2015, mwaka 2019 na mwaka huu 2023.
Katika hatua nyengine ameeleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekabidhi msaada wa kibinadamu kwa Serikali ya Jamhuri ya Uturuki kufuatia tetemeko la ardhi lililoikumba nchi hiyo Februari 6, 2023 na kusababisha madhara makubwa kwenye miji ya Kusini Mashariki mwa Uturuki.
Amesema kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Mhe. Lt Jen (Mst) Yacoub Hassan Mohammed, alikabidhi msaada huo kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa kwenye Taasisi inayohusika na majanga (AFAD), Bw. Muhammet Maruf Yaman, alipokea kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Uturuki.
Amesema kuwa Mhe. Balozi Jenerali Mohamed alitumia fursa hiyo kuwasilisha pia salamu za pole kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Watanzania kwa ujumla kwenda kwa Mheshimiwa Recep Tayyip Erdogan, Rais wa Jamhuri ya Uturuki na Raia wa Uturuki kufuatia madhara yaliyosababishwa na tetemeko hilo.
Hata hivyo amesema kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Dkt. Stergomena Tax (Mb.) katika mwezi Machi 2023 amezuru katika Nchi za Namibia, Afrika Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC na Malawi.
Amesema akiwa nchini Namibia Mheshimiwa Tax aliongoza Mkutano wa Tatu (3) wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JCC) katika ya nchi hiyo na Tanzania uliofanyika tarehe 8 hadi 10 Machi 2023 jijini Windhoek, Namibia.
Mkutano wa Tatu wa JCC ulifanyika katika ngazi mbili ya Makatibu Wakuu na Mawaziri. Mkutano wa Makatibu Wakuu ulikuwa na Kamati ya kujadili Masuala ya Diplomasia na Ulinzi na Usalama ikijumuisha Mambo ya Nje, Ulinzi, Usalama, Mambo ya Ndani na Sheria; Kamati ya Masuala ya Uchumi ilijumuisha Sekta za Uchukuzi, Biashara, Uwekezaji, Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Nishati, Madini, Mazingira, Utalii na Maliasili; na Kamati ya Jamii ilijumuisha Masuala ya Afya, Elimu, Vijana; Jinsia; Michezo; na Utamaduni.
Mkutano huo uliwezeshwa kusainiwa kwa Hati mbili za makubaliano ya ushirikiano baina ya Tanzania na Namibia ambazo ni: Hati ya makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya ulinzi na Hati ya makubaliano ya ushirikiano kati ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Namibia katika mashauriano ya kisiasa na kidiplomasia.