Mkurugenzi wa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa nchini Tanzania (WFP) Sarah Gordon (wa kwanza kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Idara ya Afya na Jamii ya Lishe TFNC, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mafunzo na Elimu ya Iishe TFNC Dkt. Esther Nkuba, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wasioona Tanzania Omary Itambu wakizundua vitabu vyenye ujumbe wa taarifa za lishe Bora kwa ajili ya watu wasioona.
Mkurugenzi wa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa nchini Tanzania (WFP) Sarah Gordon akimkabidhi kitabu cha nukta nundu chenye ujumbe wa lishe Bora Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wasioona Tanzania Omary Itambu.
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mafunzo na Elimu ya Lishe TFN, Dkt. Esther Nkuba akizungumza leo tarehe 21.3.2022 Jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa vitabu venye ujumbe wa lishe kwa watu wasioona.
……………………
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) kwa kushirikiana na Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) imezindua vitabu vinne vyenye ujumbe wa taarifa Lishe kwa ajili kuwasaidia Jumuiya ya watu wasioona ili waweze kupata elimu kuhusu umuhimu wa kula Lishe bora.
Vitabu hivyo vipo katika mfumo wa nukta nundu pamoja na sauti kwa ajili ya kuwasaidia Jumuiya ya watu wasioona ambao wengine hawajui kusoma na kuandika nukta nundu.
Akizungumza leo tarehe 21.3.2022 Jijini Dar es Salaam katika halfa ya uzinduzi wa vitabu venye ujumbe wa lishe kwa watu wasioona, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mafunzo na Elimu ya Lishe TFNC, Dkt. Esther Nkuba, amesema kuwa vitabu hivyo vina ujumbe muhimu wa lishe kwa watu wasioona, kwani kwa muda mrefu wamekuwa hawapata taarifa za lishe.
“Taarifa nyingi za lishe zimekuwa zikiandikwa katika maandishi, ambapo watu wasioona hawawezi kuona wala kusoma, hivyo imekuwa ni tatizo kubwa katika kupata taarifa za lishe kwa usahihi” amesema Dkt. NKuba.
Dkt Nkuba ameeleza kuwa jamuiya ya watu wasioona ni miongoni mwa watu katika jamii wasiofikiwa na elimu ya muhimu wa kula Lishe bora.
Amefafanua kuwa upatikanaji wa taarifa za lishe zimekuwa zikipatikana kwa njia ya radio, runinga pamoja na mitandao ya kijamii jambo ambalo limekuwa changamoto kwa Jumuiya ya watu wasioona.
“Ujumbe huo utawasaidia watu wasioona ambao hawajui kusoma na kuandika, malengo yetu watu wasioona watanufaika kwa kupata taarifa sahihi ambazo zitawasaisia kujenga uwelewa lishe na afya zao” amesema Dkt. Nkuba
Amebainisha kuwa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania imekuwa ikifanya jitihada za kukabiliana na utapia mlo nchini ili kuinua hali ya lishe Kwa ujumla.
Amesema kuwa miongoni mwa hatua ambazo wamechukua ni pamoja na kutoa elimu kwa jamii kuhusu utapia mlo wa aina zote.
“Katika kutekelezaji TFNC imefanikiwa kuwafikia makundi mbalimbali katika jamii wakiwemo wanawake wajawazito, wanaonjonyesha, pamoja na wanawake wenye umri wa kuzaa” amesema Dkt.Dkt Nkuba.
Imeelezwa kuwa nyenzo hizo muhimu yenye ujumbe wa lishe kwa watu wasioona, lengo ni pamoja na kuelimisha na kuhamasishaji jamii ya watu wasioona kuhusu umuhimu wa lishe bora kwa ustawi, ukuaji na maendeleo ya watoto na afya ya watu wa jamii hiyo kwa ujumla.
Ujumbe huo wa lishe umeandaliwa katika maandishi ya nukta na nundu na kwa wale wasiojua kusoma maandishi hayo basi wameandaliwa kwenye mfumo wa sauti.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wasioona Tanzania Omary Itambu, amesema kuwa leo imekuwa ni siku ya kipee kwao Kwa kupata nyenzo muhimu ambazo zinakwenda kuwa msaada kwao.
Amesema kuwa lishe ni jambo la muhimu kwani kama hauna lishe bora huwezi kufanya shughuli za kiuchumi.
“Wakati umefika TFNC kufanya Jambo hili kubwa na tunaomba taasisi nyengine kuiga Jambo hili lenye manufaa na kuacha alama kubwa kwetu” amesema Itambu.
Hata hivyo amewaomba wadau mbalimbali waweze kujitokeza na kusambaza ujumbe huo kwa watu wasioona katika Mikoa mbalimbali.