Chuo Cha Muhimbili leo kimeendesha kongamamno la kujadili utafiti unaohusiana na Ugonjwa wa Uviko 19 ili kuona namna ulivyosababisha athari kwa Afya ya jamii na kiuchumi kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamamno hilo Rais wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibari Dkt. Hussein Ally Mwinyi amehimiza watafiti kuhakikisha tafiti wanazozifanya zinawafikia wananchi ili kuweza kuboresha Afya zao.
“Matokeo ya utafiti ili yawe natija ni muhimu matokeo ya utafiti yawafikie watunga sera ili waweze kuandaa sera za kutatua changamoto mbalimbali zinazohusu majanga ya kiafya” amesema Rais Dkt Mwinyi.
Aidha Rais Dkt Mwinyi amefafanua kwamba tafiti hizo zipatazo nane zimefanya na Wanasayansi wa chuo kikuu cha Sayansi na Tiba shirikishi Muhimbili ( MUHAS) kwa ufadhili wa msaada wa familia ya Hayati profesa Amnen Salim ambaye alikua ni mke wa Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania ikiwa ni sehemu ya Kumbukumbu ya kumuenzi Hayati Mama Amnen Salim.
Dkt.Mwinyi amesema kwamba familia hiyo inakukumbusha kutambua jukumu la kila mmoja kutambua mchango wake kwa Taifa katika kukabiliana na majanga mbalimbali ya kiafya na kiuchumi.
Kwa upande wake makamu mkuu wa chuo cha Muhas Profesa Profesa Adrean B. Pembe amesema anaishukuru familia Salim Ahmed Salim kwa kufadhili wanasayansi wa chuo hicho kufanya utafiti wa ugonjwa wa Corona hapa nchini ambapo utafiti huo ulianza Oktoba 2021, ambapo ulifanywa na wanasayansi nane.
Utafiti huo umesaidia Umma kupata taarifa, takwimu na ufahamu zaidi kuhusu ugonjwa wa uviko 19, tafiti hizo pia zimeendelea kuboresha matibabu sera na uelewa kwa wataalam kuendelea na mapambano dhidi ya ugonjwa huo na kuweka mazingira ya kujiandaa na janga lolote linaloweza kutokea hapa nchini.
Kwa upande wao baadhi ya Wanasayansi walioshiriki utafiti huo ikiwemo Dkt. Alphonciana Kagaigai ambaye amefanya utafiti wa Afya ya akili kwa upande wa wahudumu Afya amesema kwamba kwa kiasi kikubwa wahudumu wa Afya wameathirika kiasaikolojia kutokana na kuhudumia wagonjwa wa Uviko 19.
Nae Dkt. Mourice Mbunde aliefanya utafiti wa matumizi ya dawa za asili katika kipindi cha mlipuko wa Ugonjwa wa Covid 19 amesema kwamba asilimia kubwa ya wananchi walitumia madawa ya asili kwa kujifukiza na kunywa hali iliyosaidia kipunguza makali ya maambukizi.