Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya, akizungumza na wananchi wa Wilaya
ya Rufiji (hawapo pichani) mara baada ya kuweka saini mikataba wa ujenzi wa barabara
ya Nyamwage hadi Utete (km 33.7) kwa kiwango cha lami na ujenzi wa Daraja la
Mbambe (m 81) na barabara unganishi (Km 3), wilayani humo mkoani Pwani.
Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya, akiwa na Mbunge wa Rufiji ambaye
pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa, wakishuhudia utiaji saini
mkataba wa ujenzi wa barabara ya Nyamwage hadi Utete (km 33.7) kwa kiwango cha
lami kati ya Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS) na Mkandarasi
kutoka Kampuni ya China Railway Seventh Group, wilayani Rufiji mkoani Pwani.
Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya (kulia) akiongozana na Mbunge wa
Rufiji ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa, katika hafla
ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa barabara ya Nyamwage hadi Utete (km 33.7) kwa
kiwango cha lami pamoja na ujenzi wa Daraja la Mbambe (m 81) na barabara unganishi
(Km 3), wilayani Rufiji mkoani Pwani.
Muonekano wa sehemu ya barabara Nyamwage hadi Utete (km 33.7) ambayo mkataba
wa ujenzi wake kwa kiwango cha lami umesainiwa na kushuhudiwa na Naibu Waziri wa
Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, wilayani Rufiji mkoani Pwani.
Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya, akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa
Pwani, Aboubakar Kunenge, katika hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa barabara
ya Nyamwage hadi Utete (km 33.7) kwa kiwango cha lami pamoja na ujenzi wa Daraja la
Mbambe (m 81) na barabara unganishi (Km 3), wilayani Rufiji mkoa wa Pwani.
Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya, akiwa na Mbunge wa Rufiji ambaye
pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa, wakishuhudia utiaji saini
mkataba wa ujenzi wa Daraja la Mbambe (m 81) na barabara unganishi (km 3), kati ya
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS) na Mkandarasi kutoka Kampuni
ya Nyanza Road Works, wilayani Rufiji mkoani Pwani.
………………………………….
Wananchi wa Wilaya ya Rufiji mkoa wa Pwani wametakiwa kutumia fursa ya ujenzi wa
barabara za lami ili kukuza biashara.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya mara baada
ya kushuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi wa barabara ya Nyamwage hadi Utete (km
33.7) kwa kiwango cha lami pamoja na ujenzi wa Daraja la Mbambe (m 81) na barabara
unganishi (Km 3) kati ya Wakala wa Brabara (TANROADS), na kampuni za China
Railway Seventh Group na Nyanza Road Works ya Tanzania.
"Ujenzi wa barabara hii na daraja utafungia fursa za usafirishaji wa abiria, mizigo,
mazao ya biashara, misitu na kuvuta watalii hivyo hii iwe chachu kwa wakazi kufungua
biashara mbalimbali zitakazoinua uchumi wa Wilaya hii", amesema Eng. Kasekenya.
Amesema ujenzi huu ni mkakati na miapango ya Serikali ya Awamu ya Sita ya
kuboresha miundombinj ya barabara na madaraja nchini ili kuondoa kero kwa
wananchi na kuunganisha barabara za mikoa na wilaya ya nchi nzima.
Aidha, ameongeza kuwa ujenzi wa barabara pamoja na daraja hilo utatumia fedha za
ndani kwa asilimia mia moja hivyo jukumu la kulinda vifaa vya ujenzi na kuvitunza ni la
kila wananchi ili viweze kuleta matokeo chanya kwa Wilaya.
Ametoa agizo kwa TANROADS kuhakikisha anawasimamia wakandarasi hao
ikiwezekana mradi ukamilike kabla ya wakati na kwa thamani halisi ya fedha.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Rufiji ambaye ni Waziri wa Maliasili na Utalii,
Mohamed Mchengerwa, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutoa takriban
bilioni 70 kwa ajili ya mradi huo kwani utaifungua Rufiji na kuifanya kuwa kituo cha
maendeleo kwa mkoa wa Pwani.
Wananchi wameisubiri barabara hii ijengwe kwa kiwango cha lami tangu mwaka 1970
bila mafanikio na kwa ujenzi huu Rais Samia ameingia mioyoni mwa wana Rufiji",
amesema Mchengerwa.
Akitoa taarifa ya mradi Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Eng.
Rogatus Mativila ameeleza kuwa ujenzi wa barabara hiyo utajengwa na mkandarasi
kutoka Kampuni ya China Railway Seventh Group Co., Ltd. ya nchini China kwa
gharama ya Shilingi TZS 43,419,537,043.19, bila kujumuisha kodi ya ongezeko la
thamani (VAT) kwa muda wa Miezi 24 na huku ujenzi wa Daraja la Mbambe utajengwa
na Mkandarasi kutoka Kampuni ya Nyanza Road Works Ltd ya Tanzania kwa gharama
ya Shilingi 24,164,904,622.00 kwa muda wa miezi 24.
Ameongeza kuwa daraja hilo litakuwa na upana wa mita 10.5 ambapo mita 7.5
zitatumika kwa ajili ya kupita magari na mita 2.5 kwa ajili ya waenda kwa miguu na
waendesha baiskeli.
Akitoa salam za Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Aboubakar Kunenge, ameishukuru
Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi na maboresho ya
miundombinu inayoendelea mkoa wa Pwani na kuwahakikishia wakandarasi kuwa
mkoa huo uko salama na watakuwa pamoja nao wakishirikiana.