KAMATI ya Kuduma ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imesema imeridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa kiwanda cha mipira ya mikono cha Bohari ya Dawa (MSD) kilichopo Idofi mkoani Njombe hivyo kuahidi kwenda kuishauri serikali kuongeza bajeti ya sh bilioni 12, kuwezesha kiwanda kuanza kazi ifikapo Julai mwaka huu.
Akizungumza jana mkoani Njombe eneo la Idofi kilichopo kiwanda hicho Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya PAC Japhet Hasunga, alisema kamati imeridhika na maendeleo ya ujenzi wa kiwanda hicho na kushauri bodi ya wakurugenzi wa MSD wawe wabunifu kufikia adhima ya serikali ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kufikia uchumi wa viwanda.
“MSD wameonyesha kwa vitendo kufikia uchumi wa vwianda, serikali na bunge tutahakikisha tunawaunga mkono na kuelekeza wawe wabunifu zaidi, viwanda vingi vianzishwe kuwezesha upatikanaji wa ajira,”alisema.
Alisema, kutokana na tathimini ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), inaonyesha ujenzi wa kiwanda umefikia asilimia 70,ambapo kamati imeona haja kwa hatua zilizobaki taasisi za udhibiti kuhakikisha zinashirikiana ipasavyo kuwezesha bidhaa zitakazozalishwa kukidhi viwango vya kimataifa.
“Kamati iliamua kuja kutembelea kiwanda hiki cha MSD, kinachofanyiwa uwekezaji na serikali kwa ajili ya kuanza kuzalisha ‘gloves’ na bidhaa nyingine ikiwemo dawa za maji, tuliletewa taarifa bungeni tumekuja kujiridhisha kuwa bajeti iliyopitishwa na bunge kama utekelezaji wake unaendana na malengo yaliyokusudiwa.
“Tumeona matumizi yaliyofanyika na baadaye kuwa na fursa ya kuishauri bunge na serikali kuhusu kilichofanyika katika matumizi ya fedha hizo za umma,”alisema.
Hasunga aliongeza kuwa, PAC katika ziara hiyo jambo muhimu ilikuwa ni kuangalia matumizi ya fedha zilizotolewa zilivyotumika na ndio sababu ya kutumia muda mrefu kuangalia kifungu kimoja kimoja na baadaye wamepokea maombi ya uongozi wa MSD kuomba serikali sh. bilioni 12, lengo likiwa ni kukamilisha ujenzi huo ambao unatarajiwa kukamilika na kiwanda kuanza uzalishaji ifikapo Julai mwaka huu.
Alisisitiza kuwa baada ya kuridhika na mchanganua wa matumizi ya awali katika taarifa walizopewa watalichukua suala la MSD kuongezewa fedha hizo na kulishauri bunge na serikali, lengo likiwa ni kukijengea uwezo kiwanda hicho kiweze kuzalisha kwa wakati na kupunguza mahitaji ya bidhaa za afya yaliyopo.
Aliongeza kuwa, kwa kuwa eneo hilo litazalisha aina mbalimbali za bidhaa za afya kwa kuanza na kiwanda cha mipira ya mikopo na baadaye kuzalisha dawa za maji na dawa aina mbalimbali za vidonge.
Alieleza kuwa mahitaji makubwa ya uzalishaji yaliyopo ni mipira inayotokana na miti ya utomvu ambapo tayari mazungumzo na wazalishaji wa bidhaa hizo mkoani Njombe, Tanga na Zanzibar yanaendelea ikiwemo kuwawezesha wananchi kulima kwa wingi.
Alisema uzalishaji wa kiwanda hicho ni fursa ya kipekee kwa wananchi kushirikiana na wataalamu kupewa mbegu kuzalisha malighafi inayohitajika, kuweza kuondokana na utegemezi wa malighafi kutoka nje, kutengeneza ajira, kupunguza umaskini na kukuza uchumi.
Naye Mwenyekiti wa Bodi wa MSD, Rosemary Silaa, alisema bohari hiyo katika kuhakikisha inatimiza majukumu yake manne, ambayo ni kununua, kutunza, kusambaza na kuzalisha wameishukuru kamati ya bunge kutembelea eneo hilo la kiwanda ambapo uzalishaji wake unatarajiwa kuanza Julai mwaka huu.
Alisema, uwezo wa uzalishaji wa kiwanda ni kufikia asilimia 83 ya mahitaji ya mipira ya mikono nchini ambapo, bodi itahakikisha inaisimamia ipasavyo MSD kufuata kanuni, taratibu na sheria.
“Niwashukuru viongozi wa bohari hiyo chini ya mkurugenzi wake Mavere, kama mlivyosikia kwa sasa tunaenda kutekeleza mkakati wa kampuni tanzu itakayosimamia shughuli nzima ya uzalishaji na MSD kubaki na wajibu wake wa kununua, kutunza na kusambaza bidhaa za afya, hapa Idofi tutaanza na ‘gloves’ ambapo mashine tayari zimeshafungwa na uzalishaji wa awali na baadaye kuzalisha bidhaa nyingine za mpira ikiwemo kondomu,”alisema.
Rosemary, alisema ili kuhakikisha hawaagizi bidhaa za mipira nje watahakikisha wanawezesha wakulima ambapo, mchakato umeshaanza ikiwemo kuzungumza nao kuweza kufikia sera ya viwanda nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa MSD Mavere Tukai, alisema wamewasilisha katika kamati hiyo taarifa ya mradi na kuomba ongezeko la fedha ili kiwanda kiweze kuanza uzalishaji ipasavyo.
“Tutaanza uzalishaji wa awali lakini bado kuna uhitaji wa fedha kuweza kukamilisha mahitaji ya kiwanda, tumezungumza na wabunge ambao wameonyesha kurudhishwa na hatua iliyopo na sisi tumewaomba wawe mabalozi wetu bungeni na serikalini,”alisema.