…………………..
Mwandishi wetu, Babati
Askari wa wanyamapori katika eneo la Jumuiya ya hifadhi ya Wanyapori ya Burunge na askari wa wanyamapori Wilaya ya Babati, Mkoa Manyara, wameanza kujengewa uwezo jinsi ya ukamataji wa majangili, kupeleleza na kufanya upekuzi.
Mafunzo ya askari hao, yameandaliwa na Mamlaka ya Usimamizi wanyamapori nchini (TAWA) na kudhaminiwa na Taasisi ya chemchem association, ambayo imekuwa ikiendesha shughuli za Utalii na uhifadhi katika eneo la Burunge WMA.
Wakitoa mafunzo hayo, Mwendesha mashitaka wa TAWA, Getrude Kariongi na mwendesha mashitaka kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa mashitaka (DPP) mkoa wa Manyara, Brandina Msawa wamewataka askari hao,kuzingatia sheria katika ukamataji wa majangili.
Kariongi amesema kama askari hao wakikamata wa majangili na kufanya upekuzi vizuri na kuhifadhi vizuri ushahidi kesi za ujangili zitasikilizwa kwa wakati na hukumu kutolewa.
Msawa amewataka Askari hao, kuzingatia sheria katika ukamataji, upelelezi na upekuzi ili kurahisisha mwenendo wa kesi za ujangili katika maeneo yao.
Awali Afisa Mhifadhi kutoka TAWA Kanda ya kaskazini, Emmanuel Pius amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa askari hao, ili kuimarisha vita dhidi ya ujangili.
Amesema Maafisa hao, pia watapatiwa elimu na polisi idara ya upelelezi jinsi ya kutoa ushahidi mahakamani na hivyo, kurahisisha usikilizwaji wa kesi.
Pius amesema ni jukumu la askari hao, kuhakikisha wanaendelea kuzilinda maliasili za taifa kwa faida ya sasa na vizazi vijavyo.
Mkuu wa idara ya ulinzi ya taasisi ya Chemchem association, Erick Nayman amesema eneo la Burunge WMA kumekuwepo na matukio ya ujangili kutokana na ongezeko shughuli za kibinaadamu ndani ya hifadhi.
Hata hivyo, amesema Chemchem kwa mwaka imekuwa ikitumia zaidi ya sh 400 milioni katika kupambana na matukio ya ujangili, ikiwepo ununuzi wa magari na vifaa vya ulinzi.
Akifungua mafunzo hayo, Katibu Tawala wilaya ya Babati, Khalfani Matipula akifungua mafunzo hayo, amewataka askari wa wanyamapori kufanyakazi kwa weledi kuhakikisha rasilimali za Taifa zinalindwa.
Amesema ni lazima vitendo vya ujangili vikomeshwe katika wilaya hiyo kwa kuhakikisha watuhumiwa wanatakamatwa na kufikishwa mahakamani kwa wakati.
MWISHO