Na Mwandishi wetu – Iringa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti Mhe. Japhet Hasunga (Mbunge) siku ya Jumanne, tarehe 14 Machi 2023 ilifanya ziara ya kukagua mradi wa upanuzi wa kituo cha kupokea, kupoza na kusafirisha umeme mkubwa cha Tagamenda Iringa ujulikanao kama “Backbone Transmission Investment Project (BTIP) awamu ya pili na kujionea namna mradi huo utakavyotekelezwa.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Japhet Hasunga (Mbunge) amesema Kamati yake imefanya ziara hiyo ili kuona na kutaka kujiridhisha juu ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi wa “BTIP” ambao unahusisha kuviongezea uwezo vituo vya kupokea na kupoza umeme mkubwa katika mikoa ya Iringa, Singida, Dodoma na Shinyanga kutoka umeme mkubwa wa Kilovoti 220 kwenda umeme mkubwa wa kilovoti 400.
Leo hii tumekuja kama Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa ajili ya kutembelea huu mradi ambao unajulikana kama mradi wa “Backbone” lengo hasa la Kamati ni kutaka kujiridhisha ni lini mradi huu utaanza kujengwa na kukamilika. Sasa tumekuja kujionea kwamba mradi ulishaanza kutekelezwa na nguzo zilishasimikwa na vyuma vimeshasimikwa kila mahali na vimekamilika na tayari sasa wanaanza kujenga ile substation kubwa ambayo itapokea kilovoti 400 kwa hiyo tulikuwa tunajiridhisha ni sehemu gani umeme wa kilovoti 400 itajengwa na tumeshajionea na tumeona lakini pia nyuma yetu tumeona kwamba kuna umeme ambao ni kilovolti 220 ambao tayari umeshakamilika alisema Mhe. Hasunga.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Bw. Maharage Chande amesema mradi wa “Backbone Transmission Investment Project (BTIP)” umekamilika kwa awamu ya kwanza iliyohusu ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme mkubwa wa kilovoti 400 kutoka Iringa hadi Shinyanga yenye urefu wa Kilomita mia sita na sabini (670km) na upanuzi wa vituo vya kupokea na kupoza umeme mkubwa wa kilovoti 220 kwenye mikoa ya Iringa, Dodoma, Singida na Shinyanga ambapo mpaka sasa kituo kinapokea umeme kutoka katika mabwawa ya Kidatu, Kihansi na Mtera.
“Mradi huu umekamilika kwa awamu ya kwanza kwa maana ya kituo cha kilovoti 220 na kinapokea sasa umeme kutoka katika vituo vya kuzalisha umeme kwa maji vya Mtera, Kidatu, na Kihansi. Kituo hiki kina manufaa makubwa ya kuwezesha nchi yetu kuwa na umeme wa uhakika na wenye ubora kwani kituo hiki kikikamilika kitaweza kupeleka umeme kwenye zaidi ya mikoa 18 ambayo sasa hivi inapata umeme kutoka kwenye kituo hiki alisem Bw. Chande
Bw. Chande aliongeza kuwa mradi huu wa upanuzi utakapokamilika utawezesha kupeleka umeme katika nchi zilizopo Kusini mwa bara la Afrika (SADC) ambapo kwa sasa kuna fursa kubwa ya kuuza umeme.
“Lakini vilevile kituo hiki ni kitovu cha kupeleka umeme katika nchi za “Southern African Power Pool (SAPP) kupitia nchi ya Zambia ambapo kwa sasa hivi kuna fursa kubwa sana za kuuza umeme kwa sababu umeme kwa upande huo umepungua lakini pia kuunganisha nchi za upande wa Mashariki Eastern African Power Pool (EAPP) kupitia nchi za Kenya, Uganda na Ethiopia. Kwa hiyo awamu ya pili ya upanuzi wa kituo hiki ambapo sasa kitapelekwa kwenye kilovoti 400 kitawezesha kupeleka umeme katika nchi za Kusini mwa bara la Afrika (SADC) alifafanua Bw. Chande.
Bw. Chande aliendelea kufafanua kuwa mradi huu unategemewa kuanza kutekelezwa hivi karibuni.
Mradi huu unategemewa kuanza kutekelezwa hivi karibuni kwani tupo katika hatua za manunuzi ambapo tunategemea mpaka mwezi wa nne au wa tano zitakuwa zimeshamilika na kuanza kupata mkandarasi wa kuanza kujenga kituo hiki cha upanuzi na njia kuu za kupeleka katika kituo kinachofuata cha Kisada, na Iganjo, ili umeme uweze kusafiri na kuweza kufika , alihitimisha Bw. Chande.
Mradi huu wa “Backbone Transmission Investment Project (BTIP)” awamu ya pili unahusisha kukiongezea uwezo kituo cha kupokea na kupoza umeme mkubwa cha Tagamenda -Iringa kwa kusimika mashine umba (transfoma) mbili zenye uwezo wa MVA 250 kila moja. Hapo awali, utekelezaji wa mradi huu ulikuwa sehemu ya mradi wa “backbone” awamu ya pili na ulikuwa ufadhiliwe na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (The European Investment Bank – EIB) kwa dola za marekani milioni 60 lakini kwa sasa mradi huu unatekelezwa kupitia mradi wa Tanzania-Zambia (TAZA) kwa ufadhili wa Benki ya Dunia.
Mradi huu utakiongezea uwezo kituo cha kupokea, kupoza na kusafirisha umeme mkubwa kutoka umeme mkubwa wa kilovoti 220 kwenda umeme mkubwa wa kilovoti 400 hali itakayowezesha kuongeza uwezo wa kusafirisha umeme mkubwa kwenda mikoa ya Kusini mwa Tanzania ili kuiunganisha Tanzania na nchi jirani za kusini mwa bara la Afrika kupitia mradi wa Tanzania-Zambia na hii itawezesha kuwauzia umeme nchi jirani na hivyo kuongeza pato la taifa.