Na Mwandishi wetu, Simanjiro
KUNDI la wafaransa 20 wamejitolea madawati 30 viti 20 na meza 20 kwa ajili ya shule ya msingi Saniniu Laizer iliyopo kijiji cha Naepo Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, iliyokuwa na upungufu wa samani hizo.
Mmoja kati ya wafaransa hao Jean Claude Petit akizungumza baada ya kukabidhi samani hizo amesema wao hujihusisha na masuala ya madini ikiwemo usonara hivyo wakaamua kutoa msaada huo.
“Tulifika kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite tukasikia sifa za bilionea Saniniu Laizer kujenga shule na kuikabidhi serikali hivyo tukaamua kuisaidia madawati, viti na meza hizo,” amesema Petit.
Amesema wana uzoefu wa sekta ya madini kwa miaka 25 na walipofika Januari 2023 kwa mara ya kwanza kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite walisikia sifa za shule hiyo na kupanga kuisaidia.
Bilionea Saniniu Laizer aliyejenga shule hiyo iliyopo kitongoji cha Namelock kijiji cha Naepo kata ya Naisinyai kwa gharama ya sh466.8 milioni na kuikabidhi Serikali Januari 2021 amewashukuru wafaransa hao.
“Watoto wa wakulima na wafugaji wadogo ndiyo wanaosoma shuleni hapa hivyo kitendo cha kutoa samani hizi ni cha kupongezwa ili kuondoa changamoto hiyo,” amesema bilionea Laizer.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Simanjiro, Kiria Laizer ambaye alichangia mifugo 200 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa bweni la shule hiyo amewashukuru wageni hao kwa msaada huo.
Diwani wa kata ya Naisinyai, Taiko Kurian amesema msaada huo utasaidia kuondoa changamoto ya viti iliyokuwa inawakabili wanafunzi hao hivyo amewashukuru wageni hao.
Kaimu afisa elimu msingi wa halmashauri ya wilaya hiyo, Abdalah Hamis amewashukuru wafaransa hao kwa kuwapa watoto hao samani hizo watakazokuwa wakizitumia.
Mmoja kati ya wanafunzi wa shule hiyo Elias Joseph amewashukuru wafaransa hao kwa kujitoleamsaada huo utakaowasaidia wanafunzi hao kusoma kwa bidii.