Adeladius Makwega-Zanzibar
Kamati ya Kuratibu Upatikanaji wa Vazi Rasmi la Taifa chini ya Uenyekiti wake wa Profesa Hermas Mwansoko Machi 14, 2023 imekutana na wananchi wa Zanzibar katika kukusanya maoni hayo juu ya mchakato wa kulipata vazi hilo katika mkutano maalumu uliofanyika katika Ofisi za Baraza la Sanaa Zanzibar hapa Mwanakwerekwe.
Akizungumza katika kikao hicho Mwenyekiti wa Kamati hiyo Profesa Mwansoke amesema kuwa wao wapo hapo kukusanya maoni je kitambaa hicho cha vazi hilo kiweje na kinashonajwe?
“Nawaombeni toeni maoni yenu kwa uhuru mkubwa, kwa utulivu mkubwa na kwa amani tele kwa maaana maoni ya Zanzibar yana umuhimu mkubwa kwani suala hilo ni la pande zote za muungano wa Tanzania. Vazi hilo ifahamike wazi litavaliwa kwa hiari ya kila mmoja, serikali haiwezi kufanya shuruti la Mtanzania kuvaa vazi hilo, hivyo maoni lazima tuyatoe kwa mapenzi tele ya taifa hili.”
Akizungumza katika ukusanyaji wa maoni hayo Dkt. Emmanuel Temu ambaye ni Katibu wa Kamati hiyo iliyoundwa na waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo hapo awali ambaye pia ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni nchini amesema kuwa wapo hapo kupokea maoni ya wazi hilo ambayo pia yalishakusanywa kupitia madodoso kadhaa na kupitia barua pepe na nambari za simu ambazo pia zilisambazwa awali.
Mwandishi wa ripoti hii alishuhudia maoni kadhaa yakitolewa katika ukumbi huo kwa uhuru mkubwa na wajumbe wengi akiwamo ndugu Mohammed Jahariya aliyesema wazi kuwa maoni yote ya vazi anayakubali lakini aliomba kamati hiyo itazame namna ya vazi la taifa lishonwe kwa kwa kufumwa kama walivyofanya mababu na mabibi wa taifa letu .
Naye Bi Ummi Katibu alisema kuwa wala sasa si wakati wa kupoteza muda kitambaa hicho kiweje bali kazi hiyo ilifanywa tangu enzi katika bendera ya taifa la Tanzania sasa bendera itumike kama ilivyo na kuwa kitambaa cha vazi hilo,
“Suala la kushona kama mtu anataka gauni, haya kama kuna mtu anataka kanzu sawa, kama mtu anataka baibui hilo ni shauri yake mvaaji. Rangi hizo za bendera zinaweza kuwekwa katika ua lililochorwa katika kitambaa hicho.” Alimalizia Bi Ummi Katibu.
Akizungumza awali wakati wa ufunguzi wa kikao hcho kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar Dkt. Abdallla Adam ambaye pia ndiye Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Zanzibar aliwaambia Wazanzibar kadhaa waliojitokeza katika ukumbi huo kuwa wawe uhuru kutoa maoni yao
“Hii ni nchi yetu na Vazi la Taifa litakuwa amali yetu kwa hiyo tusisite kuyataja mapendekezo yetu.”
Mkutano huu wa Zanzibar ni sehemu mojawapo wa ukusanyaji wa maoni katika mikoa saba ya kanda ambazo ni Mtwara, Dodoma, Mbeya, Dar esSalaam, Arusha, Mwanza na Tanga huku kikao hicho cha Zanzibar kikikusanya wajumbe zaidi ya 100.
Wajumbe wengine waliongozana na Profesa Mwansoko hapa Mwanakwerekwe Zanzibar ni Chifu Antonia Sangali(mwakilishi wa Machifu), Hadija Mwanamboka(mbunifu mitindo),Mustafa Hasanali(mbunifu mitindo), Mrisho Mpoto(Msanii) na Masoud Ally maarufu kwa jina la Kipanya(msanii wa uchoraji na usanifu).