Na WAF- Dodoma
Wauguzi nchini wametakiwa kuzingatia kiapo cha maadili katika kutekeleza majukumu yao ili kuhakikisha huduma bora za afya zinatolewa kwa wananchi.
Wito huo umetolewa leo tarehe 13 Machi, 2023 na Katibu Mkuu Dkt. Seif Shekalaghe wakati akifungua Mkutano wa Wauguzi na Wakunga Viongozi unaofanyika jijini Dodoma.
Dkt. Shekalaghe amesema Wauguzi na Wakunga ni jeshi kubwa ambalo liko mstari wa mbele katika kuhudumia mgonjwa toka anapoingia Hospitali kupata matibabu mpaka anaporuhusiwa hivyo amewataka kuendelea kuwa na moyo wa huruma wanaouonyesha licha ya kuwa na changamoto mbalimbali zinazowakabili.
“Upendo unasaidia sana kujenga umoja baina ya watoa huduma, hivyo ninawaomba sana wauguzi kuwa na umoja na kushirikiana na kada mbalimbali ambazo zinashirikiana katika kutoa huduma, najua kuna changamoto mnazokutana nazo lakini zisiwe chanzo cha kuwakatisha tamaa bali ndiyo iwe chachu ya kupambana zaidi”. Amesema Dkt. Shekalaghe.
Hata hivyo, Dkt. Shekalaghe amewataka wauguzi hao kuzingatia huduma kwa wateja kwani ndiyo chachu ya kutoa huduma bora na kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi.
“Siku zote sisi Viongozi uwa tunasisitiza watoa huduma wawe na huduma bora kwa wateja, bila kuwa na huduma bora malalamiko hayawezi kuisha kutoka kwa wananchi lakini mkumbuke kuwa taswira ya afya nchini imebebwa na wauguzi”. Ameongeza Dkt. Shekalaghe.
Kwa upande Mkurugenzi wa huduma za uuguzi na ukunga kutoka Wizara ya Afya Bi. Ziada Sellah amesema lengo la mkutano huo ni kutoa mafunzo mahususi kwa wauguzi viongozi ya kuwezesha kusimamia huduma za afya ya mama na mtoto, stadi za uongozi na kusimamia maadili ya taaluma pamoja na mikakati ya Kwenda kuhakikisha elimu ya Bima ya afya kwa wote inatolewa kwa umma.