Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Malisili na Utalii. Kulia ni Naibu Waziri Geofrey Pinda na kushoto ni Katibu Mkuu Anthony Sanga.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Malisili na Utalii Timotheo Msava akisisitiza jambo katika kikao cha kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi jijini Dodoma tarehe 12 Machi 2023.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Malisili na Utalii wakifuatilia uwasilishwaji taarifa ya utekelezaji majukumu ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi jijini Dodoma tarehe 12 Machi 2023.
Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa Hamad Abdallah akieleza mbele ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Malisili na Utalii hatua ambayo Shirika lake limefikia kwenye ujenzi wa soko la Madini ya Tanzanite wakati wa kikao cha kamati hiyo jijimi Dodoma.
Mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Malisili na Utalii akisisitiza jambo wakati wa kuchangia mada juu ya utekelezaji majukumu ya Wizara ya Ardhi.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akisisitiza jambo katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii jijini Dodoma tarehe 12 Machi 2023.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Lucy Kabyemera (kushoto) akiwa na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii wakati wa kikao jijini Dodoma tarehe 12 Machi 2023.
……………………………………
Na Munir Shemweta, WANMM
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imewasilisha na kujadili taarifa ya utekelezaji majukumu yake kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Malisili na Utalii.
Akizungumza wakati wa uwasilishaji taarifa ya utekelezaji mbele ya Kamati hiyo leo tarehe 12 Machi 2023 jijini Dodoma, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula mbali na kuwaeleza wajumbe wa Kamati hiyo ambao wengi wao ni wapya muundo na majukumu ya Wizara, alielezea maendeleo ya utekelezaji wa miradi inayofanywa na Wizara pamoja na taasisi zilizo chini ya wizara ya Ardhi.
Kamati ya Ardhi Maliasili na Utalii kwa sasa inaoongozwa na Mbunge wa Jimbo la Korogwe Timotheo Mzava huku Makamu Mwenyekiti wake ni Mbunge wa jimbo la Kondoa Ally Juma Makoa ambaye awali alikuwa mwenyekiti wa Kamati hiyo.
Akizumgumza kwa mara ya kwanza kama Mwenyeki wa Kamati ya Ardhi Maliasili na Utalii Timotheo Mzava amewataka wajumbe wa kamati pamoja na wizara kumpa ushirikiano katika kipindi chote cha utekelezaji wa majukumu ya kamati ili kufanikisha kazi na kusisitiza kuwa, ushirikiano ndiyo njia bora ya kuja na matokeo chanya.
Kupitia Kamati hiyo ya Bunge, Waziri Mabula alieleza miradi inayotekelezwa na wizara yake kuwa ni pamoja na ule wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK), program inayotekelezwa wilayani Meru mkoa wa Arusha, mradi wa ujenzi wa soko la Madini ya Tanzanite ulioko Mererani unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) pamoja na kazi ya uimarishaji mpaka wa Tanzania na Kenya katika eneo la Namanga.
Kamati hiyo ya Kudumu ya Ardhi Maliasili na Utalii inatarajiwa kutembelea miradi inayotekelezwa na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuanzia siku ya jumatano tarehe 15 hadi 18 Machi 2023 mkoani Arusha kabla ya Wizara hiyo kuwasilisha taarifa ya utekelezaji Mpango wa Bajeti (RANDAMA) kwa mwaka wa fedha 2023/2024.