Na. Mwandishi wetu Jeshi la Polisi.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limewataka waendesha baiskeli mkoani humo kutii sheria za usalama barabarani bila kushurutishwa.
Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Arusha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi SSP Sammy Magige wakati akifungua mazoezi ya waendesha baiskeli yaliyoandaliwa maalumu kwa ajili ya kutoa elimu kwa watumiaji wa barabara ikiwemo baiskeli ya namna ya utumiaji sahihi wa vyombo hivyo wakiwa barabarani.
SSP Magige amesema kupitia elimu hiyo ni imani yake kuwa waendesha baiskeli wote na hata watumiaji wa vyombo vya moto watafuata sheria za usalama barabarani pasipo kulazimishwa na hatimae kupelekea ajali za barabarani kuisha.
Naye Kaimu Mkuu wa Usalama barabarani mkoani humo mrakibu msaidizi wa Polisi ASP Adam Kimbesi pamoja na kushukuru uongozi wa waendesha baiskeli kwa kuandaa tukio hilo amesema kupitia elimu hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza ajali za barabarani na kuwaomba kuendelea kuaandaa mazoezi kama hayo mara kwa mara ili jamii ipate elimu ya kutosha.
Mwanzilishi wa kikundi cha waendesha baiskeli (Pedal Tz) mkoa wa Arusha Bwana Bashir Shaa amesema pamoja na kuendesha baiskeli pia kikundi hicho kinatoa huduma kwa jamii ikiwemo kutoa elimu ikiwemo za usalama barabarani katika kuepusha ajali.
Kwa upande wake Bwana Ramadhan Athumani kwa niaba ya waendesha baiskeli amesema wameungana ili kupaza sauti kwa jamii kupata uelewa wa pamoja kuhusu haki ya matumizi ya barabara bila kubaguana akitolea mfano watembea kwa miguu, baiskeli, pikipiki na hata magari.
Naye Sajenti Atilio Choga toka dawati la Elimu kikosi cha Usalama barabarani mkoa wa Arusha amesema kila mmoja akitimiza wajibu wake barabarani bila kushurutishwa kwa kufuata sheria ajali zitapungua ama kuisha kabisa.