Na Mwandishi Wetu, Lushoto
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndugu Abdulrahman Kinana ameongoza Waislamu wa Wilaya la Lushoto mkoani Tanga kufungua msikiti wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania( BAKWATA) Wilaya ya Lushoto.
Viongozi wa BAKWATA wakiongozwa na Mufti wa Tanzania Sheikh Dk. Aboubakari Zuberi wameshiriki tukio hilo la ufunguzi wa msikiti huo ambalo limekwenda sambamba na harambee ya uchangiaji ili kukamilisha ujenzi wa msikiti huo ambapo zinahitajika zaidi ya Sh.milioni 200 kuendeleza ujenzi wake. Msikiti huo utakapokamilika utakuwa na ghorofa tatu.
Kwa sasa awamu ya kwanza ya ujenzi wa msikiti huo unaohusisha ukumbi wa kuswalia umekamilika.
Akizungumza baada ya kuzindua msikiti huo mkubwa wa Wilaya ya Lushoto, Ndugu Kinana amewapongeza kwa hatua ya ujenzi wa msikiti huo huku akitumia nafasi hiyo kutoa ahadi ya mifuko ya saruji 300 pamoja na fedha Sh.milioni 10.
“Niwapongeze Waislamu wote wa Wilaya ya Lushoto kwa namna mlivyoshikamana ,Umoja na mshikamano wenu ambao umewezesha kujengwa kwa msikiti huu.Pia niwapongeze kwa namna mlivyoshiirikiana kupata hati ya eneo hili,naamini wakati mnaanza kujenga kuna watu walikuwa na shaka kama mnaweza kujenga lakini leo ukiingia ndani ya msikiti unaona fahari kwa jinsi ulivyojengwa.
Kwa upande wake Muft wa Tanzania Dk Aboubakari Zuberi amemueleza Kinana kwamba asili ya msikiti huo ni Maulid ya Kitaifa iliyofanyika Wilaya ya Lushoto mwaka 2004 ambapo msikiti ulikuwepo haukuwa na hadhi ya kuwa Msikiti Mkuu wa Wilaya ya Lushoto,hivyo wakati huo Mufti Sheikh Shaaban Simba na yeye akiwa Naibu Mufti walikubaliana ujengwe msikiti wenye hadhi na heshima ya Wilaya.
“Hivyo tukaanza kuweka mipango na mikakati mbalimbali ikiwemo kuunda Kamati za kusimamia ujenzi wa msikiti huu, watu wameminyana tangu mwaka 2004 kujenga msikiti na nguvu nyingi zinatumika kuweka sawa eneo hili.”amesema Mufti Sheikh Zuberi.
Awali akisoma risala ya uzinduzi wa msikiti huo Mohamed Said amesema wanashukuru Ndugu Kinana kwa kukubali kuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa msikiti huo pamoja na kuzindua harambee ya kichangia ujenzi.
Hata hivyo kwenye harambee ya ujenzi wa msikiti huo jumla ya ahadi ya fedha Sh.milioni 21.imeahidiwa, mifuko ya saruji 950 ,nondo tani tano huku pia ikitolewa akaunti namba ya NMB kwa ajili ya wanaotoka kuchangia kwa kutumia benki hiyo ambayo ni NMB 41606600253 jina BAKWATA Wilaya ya Lushoto