Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Mhe. Netumbo Nandi-Naitwa wakisaini Hati za Makubaliano ya Ushirikiano katika masuala ya ulinzi, nishati na mashauriano ya kisiasa na kidiplomasia kati ya Tanzania na Namibia jijini Windhoek Namibia.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akihutubia wakati wa Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Namibia jijini Windhoek. Katika hotuba yake amesisitiza umuhimu wa kufanyia kazi kwa wakati maazimio ya mkutano huo ili kuweza kujenga uchumi imara wa kisekta na kujenga mahusiano mazuri baina ya wananchi wa Tanzania na Namibia.
Kutoka kushoto, Naibu Waziri Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. David Silinde(Mb.) na Naibu Waziri Wizara ya Nishati, Mhe. Steven Byabato (Mb.)wakifatilia majadiliano katika Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JCC) kati ya Tanzania na Namibia uliofanyika jijini Windhoek, Namibia.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Mhe. Netumbo Nandi-Naitwa katika picha ya pamoja na Mawaziri wa Tanzania na Namibia, Makatibu Wakuu walioongoza ujumbe wa Tanzania na Namibia katika Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JCC) ngazi ya Maafisa Waandamizi na Mabalozi wa Tanzania na Namibia.
………………………………..
Windhoek, Namibia, 10 Machi 2023
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri Namibia zimesaini Hati za Makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya usalama, mishati na mashauriano ya kisiasa na kidiplomasia.
Hati za Makubaliano hayo zimesainiwa katika Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JCC) kati ya Tanzania na Namibia uliomalizika jijini Windhoek, Namibia tarehe 10 Machi 2023 katika ngazi ya Mawaziri.
Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Mkutano huu umeongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) ambaye ameambatana na Naibu Waziri Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. David Silinde(Mb.) na Naibu Waziri Wizara ya Nishati, Mhe. Steven Byabato (Mb.).
Kadhalika, ujumbe wa Jamhuri ya Namibia umeongozwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Mhe. Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah ambaye ameambatana na Mawaziri wa kisekta na Makatibu Wakuu wa nchi hiyo.
Mkutano wa Tatu wa JCC kati ya Tanzania na Namibia umejadili na kutathimini masuala mbalimbali ya utekelezaji kwenye maeneo ya ushirikiano yaliyokubaliwa baina ya nchi hizi. Maeneo hayo ni pamoja na; Siasa na Diplomasia, Ulinzi na Usalama, Uchumi, Nishati, Kilimo,
Maendeleo na Miji, Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Maliasili, Utalii na Mazingira, na Uvuvi, Afya, Elimu na Utamaduni.
Aidha, mkutano huu wa Mawaziri umewaagiza watendaji katika sekta za ushirikiano kukamilisha kwa wakati masuala yote yanayohitaji utekelezaji ndani ya muda ulioazimiwa na kikao hicho ili kuleta tija katika shughuli za wananchi na kuwainua kiuchumi.
Vilevile, wamesisitiza umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia uliopo kwa manufaa ya kiuchumi na kijamii katika ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika na Bara la Afrika kwa ujumla.
Wakihutubia katika ufunguzi wa mkutano huo Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania na Namibia Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Mhe. Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah wamesisitiza umuhimu wa kukuza mawasiliano baina nchi hizo mbili ili kuweza kurithisha kizazi cha sasa juu ya historia ya mataifa hayo mawili na kufahamu ndoto kubwa waliyokuwa nayo waasisi wa matifa haya katika kuyafikia maendeleo ya watu wake.
Mkutano huu ulitanguliwa na mkutano wa awali wa ngazi ya Maafisa Waandamizi uliofanyika tarehe 8 Machi 2023 na kufuatiwa na mkutano ngazi ya Makatibu Wakuu uliofanyika tarehe 9 Machi 2023.
Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Namibia (JCC) umeazimia kuwa mkutano ujao utafanyika mwaka 2024 nchini Tanzania.