Na John Walter-Babati
Halmashauri ya wilaya ya Babati mkoani Manyara imesema imetoa mikopo isiyokuwa na riba kwa wanawake sh. Mil. 364.5 kwa vikundi 50 kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Taarifa ya kutolewa mikopo hiyo ilitolewa jana na Ofisa maendeleo wa Halmashauri hiyo January Bikuba wakati akitoa taarifa ya idara hiyo kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani.
Alisema mikopo hiyo ilitolewa Machi mwaka jana hadi Machi mwaka huu kwa vikundi vya wanawake ili kuwainua kiuchumi.
Aidha alisema ukatili wa kijinsia bado ni moja ya ukwamishaji wa jitihada za kuinua uchumi wa wanawake.
“Kamati 25 za kutokomeza ukatili zimeundwa na kamati 15 zimeishajengewa uwezo,”alisema Bikuba
Naye Meneja mkazi Tanzania wa Shirika la So They Can Roselyne Maliki alisema walipoanza katika kata za Mamire na Endakiso walijenga chuo cha ualimu Mamire ambacho kimeishazalisha walimu 640 na asilimia 40 ni walimu wa kike.
Mariki alisema wameshakarabati madarasa 89 na kutoa madawati 770 ambapo wako vijiji 17 katika kata nne.
Vile vile alisema mtoto anatakiwa apewe haki ya kukua na kupata elimu akiwa salama.
“Tunaomba tukatae mila potofu na vibanda umiza tusikubali vibanda umiza kuwa walezi wa watoto wetu,”alisema Mariki
Pia mkuu wa kikosi cha ulinzi na usalama barabarani mkoani Manyara Georgina Matagi alisema wimbi la kulawiti liko kwa watoto wa kiume hivyo lipigwe vita kwa nguvu zote.
Akitoa hotuba kwenye maadhimisho hayo kamanda wa polisi mkoani Manyara Kamishna msaidizi wa polisi George Katabazi ambaye alikuwa mgeni rasmi alisema ni vizuri wananchi wawe wanaripoti vitendo vya ukatili wa watoto na wanawake.
Katabazi aliwaomba wanawake kuacha kukaa kimya wakati wanaonewa bali wawe makini na teknolojia kwa kufatilia simu zenye tija kwa ajili ya biashara au mambo ya kijamii.