Meneja kitengo cha uchunguzi wa saratani na elimu kwa umma ,Dk Maguha Stephano kutoka Taasisi ya saratani Ocean road   akizungumza na madaktari na wauguzi katika hospitali ya ALMC Selian kuhusu maswala ya saratani.
Baadhi ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali mkoani Arusha wakipata elimu juu ya maswala ya saratani walipofika kupata huduma hiyo katika hospitali ya rufaa ya mkoa Mount Meru.
Julieth Laizer ,Arusha.
Arusha .Wananchi mbalimbali mkoani Arusha wametakiwa kujitokeza kwa wingi kufanyiwa uchunguzi wa saratani unaotolewa bure na madaktari bingwa kutoka Taasisi ya saratani Ocean Road kwa  kushirikiana na Hospitali ya rufaa ya mkoa Mount Meru.
Aidha huduma hiyo ya matibabu ambayo ilianza machi 6 na itamalizika machi 10 tayari , Jumla ya wanawake 351 kutoka maeneo mbalimbali mkoani Arusha wamefanyiwa  uchunguzi wa saratani  ya mlango wa kizazi na matiti .
Hayo yamesemwa  jijini Arusha na Meneja kitengo cha uchunguzi wa saratani na elimu kwa umma kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road ,Dk Maguha Stephano wakati akizungumza  katika kambi  hiyo ya uchunguzi na matibabu ya saratani inayoendelea katika hospitali ya rufaa ya mkoa Mount Meru ambayo imefadhiliwa na Benki ya NBC.
Amesema ,kumekuwepo na ongezeko la  idadi ya wagonjwa wa  saratani mwaka hadi mwaka ambapo wagonjwa wengi hufika hospitali katika hatua za mwisho kabisa ambapo taasisi hiyo imeona kuna umuhimu  wa kuandaa mpango  huo na kwenda  katika hospitali hiyo kwa ajili kutoa elimu na kufanya uchunguzi wa awali wa saratani.
Dk.Maguha amesema wanawake 351 wamefanyiwa uchunguzi wa saratani ya mlango na matiti na kati yao wanawake 7 wamekutwa na mabadiliko ya awali ya  saratani ya mlango wa   kizazi na kufanyiwa matibabu huku wanawake   4 wakikutwa na viashiria vya  saratani ya   mlango wa kizazi na wengine 9 wakikutwa na vivimbe  katika matiti yao na hivyo kufanyiwa vipimo zaidi na madaktari bingwa wa Patholojia kwa uchunguzi zaidi.
“Kupitia kambi hii pia tumeweza kupima saratani ya tezi dume ambapo  jumla ya wanaume 100 wamefanyiwa  vipimo na kati ya hao  wanaume 7 wamekutwa  na viashiria vya saratani ya   Tezi dume na hivyo wanatakiwa kufanyiwa vipimo zaidi  
“amesema Dk. Maguha.
Aidha amesema kuwa,lengo  la kambi hiyo ni kutoa elimu ya magonjwa ya saratani kwa wananchi wa Arusha na kutoa huduma ya uchunguzi wa awali wa saratani bila malipo na kuwezesha ugunduzi  wa mapema wa saratani katika hatua za awali kwa wananchi wa Arusha.
“Lakini pia kupitia kambi hii ya madaktari bingwa kutoka Taasisi ya  Ocean Road tumeweza kubadilishana uzoefu  wa utendaji kazi kati ya madaktari wetu na madaktari wa hospitali ya rufaa Mount Meru na hospitali ya ALMC  Selian kuhusu magonjwa ya saratani .”
Ameongeza kuwa, kanzi data  ya Taasisi hiyo  kwa mwaka 2021 zinaonyesha kwamba wagonjwa  kwa upande wa Wanawake aina za saratani  zinazoongoza ni pamoja na saratani ya mlango wa  kizazi kwa asilimia 47,ikifuatiwa  na saratani  ya matiti  kwa asilimia 18 na saratani ya koo kwa asilimia 4 huku kwa upande wa wanaume saratani ya koo  la chakula likiongoza kwa asilimia 18 ikifuatiwa  na saratani  ya tezi dume kwa asilimia 11
Hata hivyo amesema ,njia mbalimbali za  kujiepusha na saratani ni pamoja na kupunguza matumizi ya mafuta mengi katika vyakula hasa yale ya wanyama na kupunguza unene uliokithiri na kula  matunda  na mboga mboga kwa wingi ,kufanya mazoezi  na kuepuka matumizi ya tumbaku na pombe kupitia kiasi ,huku akiwakumbusha wananchi wa Arusha kufanya uchunguzi mara kwa mara hata kama hawana dalili zozote za ugonjwa.
Baadhi  ya wagonjwa waliofika kupata huduma katika kambi hiyo, Janeth Laizer na Dismas Mollel wamesema kuwa, wanashukuru  kwa  jinsi ambavyo taasisi hiyo imeweza kujitolea na kuja kufanya matibabu ya saratani  kwani yanawasaidia  sana kuweza  kupata  matibabu ya awali na kuweza kupata matibabu mapema.