Na Selemani Msuya, Kilombero
SERIKALI wilayani Kilombero mkoani Morogoro, imesema ili kuhakikisha mchango wa Mto Kilombero kwenye uzalishaji wa umeme na kilimo unakuwa endelevu itachukua hatua kwa watu wote wanaofanya shughuli za kilimo, ufugaji na kukata miti ndani ya vyanzo vya maji na Pori la Akiba.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa wilaya hiyo, Dunstan Kyobya jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali waliopo katika ziara ya kutembelea Bodi ya Maji Bonde la Rufiji (RBWB).
Kyobya amesema Kilombero kuna wakulima na wafugaji wengi ambao wana makundi makubwa ya mifugo, hali ambayo inachangia uharibifu wa vyanzo vya maji na mazingira, hivyo amewataka kuanza kuondoka kabla kuchukuliwa hatua za kisheria.
Amesema Mto Kilombero unachangia asilimia 65 ya maji yanaoingia Bonde la Rufiji hasa kwenye usalishaji wa umeme kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere (JNHPP), hivyo watachukua hatua kali kwa mtu anayejaribu kuharibu vyanzo vya maji na Pori la Akiba ambapo limetangazwa na Serikali hivi karibuni.
“Kilombero ni eneo muhimu katika sekta ya maji, kwani asilimia 65 ya maji yanaiingia Bonde la Rufiji yanatoka Mto Kilombero, asilimi 16 yanatoka Mto Ruaha Mkuu ambao unapita hapa Kilombero, hivyo tumejipanga kulinda vyanzo hivi muhimu kwa nguvu zote,” amesema.
Kyobya amesema katika kuonesha hawatanii, hivi karibuni wamekamata ng’ombe 201 ambao walikuwa kwenye maeneo yasiyoruhusiwa kuchunga na kutaifishwa na mahakama.
“Pia kwa sasa wapo ng’ombe 148 tunawashikilia wakisubiri hukumu ya mahakama, lengo sio kuwafirisi wafugaji, bali ni tunataka vyanzo vya maji na pori la akiba litunzwe,”amesema.
Aidha, amesema katika kuweka msisitizo wa uhifadhi na utunzaji mazingira, Kilombero imesitisha utoaji wa vibali vya uvunaji miti, hadi hapo watakapojiridhisha kuwa uharibifu umepungua.
“Kauli mbinu ya mwenge mwaka huu ni tunza mazingira, okoa vyanzo vya maji, kwa ustawi wa viumbe hai na uchumi wa taifa, hivyo sisi tunataka kuitekeleza kivitendo,”amesema.
Amesema uamuzi wa Serikali kupitia Rais Samia Suluhu Hassan kutoa GN.No.64 ya kulipandisha hadhi Pori Tengefu la Kilombero kuwa Pori la Akiba Kilombero ni hatua muhimu ambayo inatoa maelekezo kwa watu wote wanaolima na kufuga kwenye maeneo oevu watoke.
Mkuu huyo wa wilaya amewataka watendaji kuanzia ngazi ya kitongoji, kijiji, mtaa, kata, tarafa na wilaya kushiriki kikamilifu kuondoa wafugaji na wakulima wanaoingia maeneo ya vyanzo vya maji na Pori la Akiba la Kilombero.
“Unajua Kilombero ina ukubwa wa mita za mraba 14,958, vitongoji 458, vijiji 110, mitaa 55, kata 35 na tarafa 5, hivyo ushirikiano ndio unaweza kukabiliana na hii changamoto ya wakulima na wafugaji kuingia kwenye vyanzo vya maji,” amesema.
Kyobya amesema kwa sasa wanaendelea na mchakato wa kuwaondoa wafugaji ambao wana mifugo mingi, ili utunzaji vyanzo vya maji uwe endelevu.
Amewataka wafugaji kuondoa mifugo yao katika Pori la Akiba la Kilombero kwa kuwapakia kwenye magari ili kuepusha kula mazao ya wakulima na kupeleka katika vijiji ambavyo katika matumizi bora ya ardhi kumepangwa maeneo ya kufuga.
“Wafugaji wenye mifugo mingi ni vema kupeleka ngome katika maeneo kulingana na mpango wa kijiji kwa matumizi bora ya ardhi kwani, hatuwezi kuvumilia uharibifu wa vyanzo vya maji,” amesisitiza.
Pia aliwataka wakulima katika bonde hilo kuondoka baada ya kuvuna mazao yao yaliyopo sasa ili kuweza kutunza mazingira ya maeneo hayo.
Kwa upande wake Ofisa Maji wa RBWB, Kidakio cha Kilombero, Mhandisi Emmanuel Lawi amesema Mto Kilombero ni muhimu kwa Bwawa la Mwalimu Nyerere kwani kiasi cha maji kwa mwaka kinachopita ni mita za ujazo bilioni 19.
Mhandisi Lawi amesema Mto Kilombero unapokea maji kutoka mito tisa mikuu ambayo ni Lumemo, Mbingu, Lwipa, Kihansi, Mnyela, Mpanga na mingine mingi.
“Kwa mwaka Mto Kilombero unapitisha maji mita za ujazo bilioni 19 ambapo ni sawa na asilimia 65 ya maji yanaingia Bwawa la Mwalimu Nyerere,” amesema.
Lawi amesema uamuzi wa upandishaji hadhi Pori la Kilombero utasaidia uhifadhi kuongezeka, huku akiwataka wananchi kuacha kuharibu vyanzo vya maji kwa shughuli za kibinadamu kama kilimo, ufugaji na uvuvi.
Naye Mkazi wa Kivukoni, Mohamed Mwanjole amesema wafugaji ndio sababu ya uharibifu wa vyanzo vya maji, hivyo kuiomba Serikali iwaondoe.
“Kinachonikera mimi ni hii jamii ya wafugaji, wanaharibu vyanzo vya maji, wanapaswa kuondoka, ili Mto Kilombero uwe salama,” amesema.