Na. WAF – Dar Es Salaam
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ameitaka Bodi ya Wadhamini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili, kusimamia utekelezaji wa ujenzi wa majengo mapya ya hospitali, uhimarishaji wa huduma za kibingwa ili kuvutia utalii tiba pamoja na utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.
Waziri Ummy aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Bodi mpya ya Wadhamini ya Hospitali ya Hospitali ya Taifa Muhimbili ambayo Mwenyekiti wake ni Dkt. Ellen Mkondya Senkoro.
“Bodi iliyopita chini ya uongozi wa Prof. Charles Majinge ilifanya mambo makubwa kwa kuanzisha huduma za kibingwa ikiwemo Upandikizaji Figo, Upandikizaji vifaa vya kusaidia kusikia na upandikizaji uloto hivyo natamani na bodi hii nayo tuje tuipime baada ya miaka mitatu katika maeneo hayo niliyoyataja” amesema Mh. Ummy
Mh. Ummy amebainisha kuwa tayari Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi ameanza kufanya maboresho mbalimbali ya miundombinu na kuhakikisha stahiki za wafanyakazi kulipwa kwa wakati jambo ambalo limeamsha ari ya kujituma miongo mwa watumishi.
“Tumepita tumejionea uboreshaji mkubwa wa miundombinu, tumeona wodi za kisasa, na pia nina taarifa kuwa wafanyakazi wanapata stahiki zao kwa wakati kwa hili nakupongeza sana Prof. Janabi natumaini kwa kushirikiana na bodi hii mambo mazuri zaidi yatakuja hapo mbeleni” amesema Mh. Ummy
Aidha ametoa wito kwa MNH kuendelea kuwajengea uwezo wataalamu wa hospitali za rufaa za mikoa (RRH) katika maeneo mbalimbali ya kibingwa ili kurahisisha hali ya upatikanaji huduma kwa wananchi
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Ellen Mkondya Senkoro ameahidi kuwa bodi hiyo itatekeleza majukumu yake wa weledi na kufuata sheria, haki na kuahidi matokeo ya haraka hivyo wananchi wategemee huduma bora ambazo zitakidhi matarajio yao.
Awali akimkaribisha Waziri wa Afya, Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi alisema kuwa kuwa katika kipindi cha miezi minne MNH imefanikiwa kuanzisha kuduma mpya mbalimbali ikiwemo kliniki ya mafuta (Lipid Clinic) na huduma za kupunguza uzito kwa kuweka puto kwenye tumbo la chakula (Intragastic Balloon)