Na. Majid Abdulkarim, Dar es Salaam
Waziri wa Afya Mhe.Ummy Mwalimu amesema tafiti zimebaini kuwa takribani Watanzania 5,800 mpaka 8,500 wanahitaji huduma za kusafisha damu (dialysis)au huduma za kupandikizwa figo.
Mhe.Ummy amebainisha hayo leo Jijini Dar es Salaam wakati akiongea na waandishi wa habari akiwa jengo la wagonjwa wanaosafishwa figo katika Hospitali ya Taifa Muhimbi ikiwa ni Siku ya Figo duniani ambapo amesema hadi kufikia Januari 31, 2023 wagonjwa 3,250 wanapata huduma ya kusafishwa damu (dialysis) na wagonjwa 335 wamepandikizwa figo.
“Kati ya wagonjwa waliopandikizwa figo, wagonjwa 103 wamepandikizwa nchini, ambapo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imepandikiza wagonjwa 70 na Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma imepandikiza wagonjwa 33”amesema Mhe.Ummy.
Aidha, amesema, Serikali imejipanga kuweka jitihada za pekee ili kudhibiti na kuzuia ugonjwa wa figo na magonjwa yasiyoambukiza kwa ujumla kwa kuimarisha afua za kinga kwa kuwa kinga ni bora kuliko tiba.
“Hapa naomba nikumbushe umuhimu wa kubadili mtindo wa maisha kwa kufanya mazoezi, kuepuka matumizi ya tumbaku na bidhaa zake, kupunguza matumizi ya vilevi na kuzingatia ulaji wa mlo kamili wenye mbogamboga na matunda ya kutosha ili kuimarisha kinga ya mwili dhidi ya magonjwa”amesisitiza Mhe.Ummy.
Pia, Waziri Ummy amehimiza kupunguza matumizi ya chumvi, sukari na vyakula vyenye mafuta mengi pamoja na kuzingatia unywaji wa maji ya kutosha angalau kiasi cha lita 2.5 ya maji kwa kila siku na kujiepusha na matumizi ya dawa ambazo hazijatolewa maelekezo ya kitaalam na daktari.
Waziri Ummy amesema takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinabainisha kuwa asilimia 10 ya watu wote duniani wanaishi na ugonjwa sugu wa figo ambapo tatizo ni kubwa zaidi kwa watu wenye umri zaidi ya miaka 75 au zaidi huku karibu nusu yao wana tatizo hili.
Kuhusu utekelezaji wa Sera ya Afya ya mwaka 2007 Waziri Ummy amesema Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, serikali imeanzisha huduma za uchujaji wa damu kwenye hospitali za mikoa 8 kwa kuzipatia mashine 49 za dialysis na kukarabati majengo kwa gharama ya Tsh.Bilioni 2.8.
Ikumbukwe kuwa,Tanzania huungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku ya Figo Duniani ambayo huadhimishwa kila Alhamis ya Wiki ya Pili ya mwezi Machi kila mwaka ambapo Jumuiya ya Kimataifa ya Nefrolojia (ISN) kwa kushirikiana na Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Figo Duniani (IFKF)ilianzisha maadhimisho haya yalifanyika kwa mara ya kwanza mwaka 2006 na kaulimbiu ya mwaka huu ni “Afya ya Figo kwa Wote-Kujitayarisha kwa yale yasiyotarajiwa ,kusaidia waliohatarini “ambayo inalenga kuongeza ufahamu na elimu wa afya ya figo na kuhamasisha wananchi kujitokeza kupima afya zao.