Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Mhe. Dkt. Linda Salekwa ameipongeza TFS alipotembelea ofisi za taasisi hiyo katika Shamba la Miti SaoHill kwa ziara ya kikazi akiwa ameambatana na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mufindi.
Amesema kuwa pamoja na shughuli mbalimbali za uhifadhi zinazofanyika katika Shamba kumekuwa na michango mingi ambayo inatolewa kwa jamii inayolizunguka Shamba ili kujenga mahusiano mazuri.
Mkuu wa Wilaya ameongeza kuwa TFS kupitia Shamba Hilo wamekuwa wakigawa miche milioni moja ya miti bure kwa kila mwaka ambapo imepelekea wananchi wengi kupanda miti kwa wingi ikiwa ni sehemu ya uhifadhi wa mazingira na kujiongezea kipato.
” Niwapongeze TFS kwa kuhakikisha miti inapandwa kwa wingi na kuhakikisha suala la uhifadhi wa miti iliyopandwa linasimamiwa ipasavyo , kwa kweli inavutia sana unapopita huko barabarani na kuona mashamba ya miti yalivyopandwa na kutunzwa vizuri”Amesema Dkt. Linda Salekwa
Ameendelea kusisitiza kuwa suala la upandaji miti linaendana na utunzaji hivyo amewataka wananchi wote kuhakikisha miti inayopandwa katika Wilaya ya Mufindi inatunzwa vizuri ili kuondokana na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikijitokeza ikiwemo changamoto ya matukio ya moto.
Sambamba na shughuli nzuri za uhifadhi zinazofanyika amesema kuwa kumekuwa na mambo mengi ambayo yanafanywa na serikali na hivyo ni vyema wananchi wakatambua shughuli zinazofanywa katika maeneo yao ili kutambua juhudi hizo.
“Raisi wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesisitiza sana kuhakikisha tunawafahamisha wananchi kazi nzuri zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita ili wananchi watambue kazi hizo kuepusha upotishaji” Amesema Mhe. Dkt Linda Salekwa
Ameongeza kuwa anafurahishwa sana na mandhari iliyopo Wilayani Mufindi kutokana na uhifadhi mkubwa uliofanywa na serikali kwa kuanzisha Shamba la Miti SaoHill ambapo imepelekea wananchi nao kupanda miti kwa wingi kwaajili ya utunzaji wa mazingira na kujiongezea kipato.
Naye Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti SaoHill akiwasilisha taarifa ya Shamba amesema kuwa TFS kupitia Shamba umekuwa ikisaidia jamii inayolizunguka Shamba ili kujenga mahusiano mazuri ambayo imepelekea ushirikiano mzuri uliopo katika suala zima la uhifadhi wa misitu.
Amesema kuwa TFS imekuwa ikitoa miche bure kila mwaka, ujenzi wa miundombinu kama barabara ,mabweni na bwalo katika shule , ofisi na ajira kwa wananchi ambapo imepelekea wananchi kupata huduma mbalimbali ikiwemo elimu ya upandaji na uhifadhi wa misitu kutokana na uwepo wa Shamba la Miti SaoHill.