Naibu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke Eugenius Hazinamwisho akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya utekelezaji katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba, 2022.
……………………
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke imefanikiwa kufanya ufatiliaji wa miradi tisa yenye thamani ya shilingi bilioni 5,915,000,000 katika sekta za elimu, afya, mifugo pamoja na masoko.
Imebainika miradi sita yenye thamani ya Sh. 5,536,000,000 ilikutwa na kasoro mbalimbali na hatua za kisheria zilichukuliwa kukabiliana na tatizo hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 9/3/2023 Jijini Dar es Salaam, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba, 2022, Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Temeke Eugenius Hazinamwisho, amesema kuwa miongoni mwa miradi iliyokutwa na kasoro ni ujenzi wa madarasa 72 Shule ya Sekondari Lumo, ambapo kuna upungufu wa ucheleweshaji wa vifaa vya ujenzi, unaofanywa na baadhi ya maafisa wa Manispaa ya Temeke.
Miradi mengine ni ujenzi wa madara shule ya sekondari ya Nzasa, ujenzi wa vyumba nane vya madarasa na matundu 20 ya vyoo shule ya sekondari Dovya, ujenzi wa majengo ya OPD na maabara ya zahanati ya Kilakala pamoja na mradi wa ujenzi wa kituo cha huduma za wagonjwa wa kifua kikuu sugu (MDR TB – MULTIDRUG RESTANCE TUBERCULOSIS) katika hospitali ya Vijibweni Kigamboni.
“Miradi hiyo ina mapungufu mbalimbali ikiwemo ucheleweshaji wa vifaa vya ujenzi hasa vifaa ambavyo vinanunuliwa moja kwa moja kutoka viwandani, ucheleweshaji wa fedha (own source) Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, ushauri umetolewa na ufatiliaji unaendelea” amesema Hazinamwisho.
Hazinamwisho ameeleza kuwa pia wamepokea malalamiko 36 yanayohusu rushwa ambapo idara mbalimbali zimelalamikiwa ikiwemo Mahakama, Polisi, NIDA, Watendaji Kata, Ardhi, Soko, Elimu, TRA pamoja na NEMC.
Amebainisha kuwa jumla ya kesi tisa zinaendelea kwa hatua ya kusikilizwa Mhakamani na kesi moja imekamilika na kuondolewa mahakamani.
“Tunaendelea kuwasihi wananchi kufuatilia elimu tunazotoa ili watu watuletee malalamiko yanayoangukia kwenye sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa sura 329, kwani bado wengi wanawasilisha kwetu masuala yasiyohusiana na sheria” amesema Hazinamwisho.
Hazinamwisho amesema kuwa Takukuru Mkoa wa Temeke wanaendelea kuimarisha juhudi za Kuzuia rushwa kwa kuongeza ushiriki wa kila mwananchi na wadau katika kukabili tatizo la rushwa katika utoaji wa huduma za jamii na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Pia amewashukuru wananchi wa Mkoa wa Temeke na Wilaya ya Kigamboni kwa kutoa ushirikiano na kuwasihi waendelee kutoa taarifa za viashiria vya rushwa ili kutokomeza vitendo hivyo ambavyo sio rafiki mbele ya jamii.