Na WAF- DSM
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya kwa imezindua kiwanda kingine cha utengenezaji wa Barakoa aina ya N95 zintazosaidia katika kujikinga dhidi ya magonjwa ya hewa katika maeneo ya kutolea huduma.
Uzinduzi huo umefanywa leo Machi 9, 2023 na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel aliyemwakilisha Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu katika Bohari ya Dawa Jijini Dar es Salaam.
“Nimekuja hapa na Balozi wa Japan kuzindua kiwanda cha Barakoa aina ya N95, ukiacha vile vingine vinavyozalisha Barakoa za kawaida, kwa kuzalisha Barakoa hizi kutasaidia katika maeneo ya utoaji huduma na kukuza uchumi wetu kwa kuziuza kwa nchi ambazo hazina uzalishaji huu.” Amesema.
Amesema matokeo haya, yanatokana na juhudi za Rais wetu Dkt. Samia za kukuza uhusiano na mashirikiano na nchi mbalimbali unaopelekea kuvutia uwekezaji katika eneo la viwanda hali itayosaidia kupunguza changamoto ya ajira na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa.
Aidha, Dkt. Mollel amesema, Serikal ya Rais Samia imeendelea kuweka mikakati mizuri ya ushirikiano baina ya sekta binafsi na sekta ya Serikali ili kusaidia ukuaji wa uchumi na kuleta matokeo chanya baina ya pande hizo.
Kwa upande wake Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Shinichi Goto ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuboresha huduma kwa wananchi hasa katika upatikanaji wa vifaa tiba vitavyosaidia katika matibabu ya wananchi.
Sambamba na hilo Mhe. Shinichi Goto amesema Serikali ya Japan itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuboresha Sekta ya afya, hasa katika upatikanaji wa vifaa tiba.