…….,…,……..
Na John Walter-Manyara
Katika kuadhimisha siku ya Wanawake duniani, watumishi wanawake wa shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Manyara wameiadhimisha kwa kupanda miti katika shule ya sekondari Hangoni iliyoko Mjini Babati ikiwa ni sehemu ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
Afisa ugavi na usafiri mkoa Manyara ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Wanawake TANESCO Kanda ya kaskazini Alfreda Nombo, amesema wameamua kupanda miti kwa kuwa uzalishaji Umeme unategemea mvua inayotokana na miti na utunzaji wa Mazingira, hivyo zoezi hilo litasaidia kukabiliana na athari za kimazingira na hatimaye mvua za kutosha kunyesha.
Nombo amesema wamepanda miti zaidi ya 80 ya aina mbalimbali.
Amesema imekuwa siku nzuri kwao kukutana wanawake kwa pamoja kuadhimisha siku hiyo Muhimu.
Mwalimu wa Mazingira Dorcas wa shule ya Sekondari Hangoni, amesema miti hiyo itawasaidia wanafunzi kusoma katika Mazingira rafiki yenye vivuli vya kutosha na kuahidi kuitunza.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani mwaka 2023, ” Ubunifu na mabadiliko ya Teknolojia, chachu katika kuleta usawa wa kijinsia”