Tukiwa tunaadhimisha siku ya wanawake duniani, NMB imeandika historia mpya kwa kuwa Benki ya kwanza Kusini mwa Jangwa la Sahara kuorodhesha hati fungani ya kijinsia katika soko la hisa barani Ulaya.
Hati fungani hiyo inayojulikana kwa jina la ‘Jasiri’ imeorodheshwa leo katika soko la hisa la Luxembourg, moja ya masoko makubwa ya uwekezaji wa mitaji duniani na ina lengo la kukusanya fedha kwa ajili ya kutoa mikopo kwa biashara ndogo na za kati zinazomilikiwa na wanawake na biashara ambazo bidhaa au huduma zake zinamgusa mwanamke moja kwa moja.
Hadi kufikia Disemba 2022, Shilingi Bilioni 74 zilizokusanywa awali kutoka kwenye hati fungani ya Jasiri zilikua zimekopeshwa kwa biashara zaidi ya 3,000 zinazokidhi vigezo hivyo.
Hatua hii ya leo itawezesha wawekezaji barani Ulaya kupata taarifa na kutambua fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo Tanzania na Afrika kwa ujumla zinazochangia malengo ya usawa wa kijinsia.
Ujumbe wa Benki ya NMB katika hafla hiyo umeongozwa na Mhazini wa Benki, Aziz Chacha alieungana na Mwakilishi wa Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Alphonce Mayala; Waziri wa Fedha wa Luxembourg, Yuricko Backes na Afisa Mtendaji Mkuu wa LuxSE, Julie Becker kugonga kengele kuashiria uorodheshwaji rasmi wa hatifungani ya Jasiri.