Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WANAWAKE katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kufanya kazi na kutumia ushawishi wao kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo kwa uadilifu na nguvu ili waache alama.
Kauli hiyo ilitolewa na Mhasibu Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, CPA Rahab Philip alipokuwa akiongelea nafasi ya mwanamke katika kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
CPA Philip alisema kuwa mwanamke kwa asili ameumbwa kuwa binadamu imara zaidi. “Hivyo, asili yetu ni uimara, hata mwanamke aweje lazima hiyo asili anayo. Ushauri wangu kwa wanawake wenzangu, tufanye kazi kwa bidii, tusonge mbele na tufanye maamuzi sahihi na tushawishi jamii kufanya mabadiliko chanya ya kimaendeleo kwa sababu tumeumbwa kuwa watu wa kushawishi mabadiliko. Tukumbuke katika kufanya shughuli zetu kuleta mabadiliko, lazima tufanye kwa uadilifu, nguvu na bidii. Nawahakikishia tukijikita katika maeneo hayo jamii itasogea na tutaacha alama” alisema CPA Philip.
Alisema kuwa mwanamke ni nguzo katika familia kwa sababu anachukua nafasi kubwa kuhakikisha familia inakuwepo na kudumu ikiwa bora. “Naamini wote mtakubaliana nami kuwa bila mwanamke hakuna familia. Hatuwezi kusema wanaume hawana umuhimu katika familia, lakini mchango wa mwanamke ni mkubwa sana. Ikitokea tu mama akaondoka ile familia lazima itayumba. Hata baba akiwepo yeye ameumbwa kuwa muwezeshaji. Hata akiwezesha mahitaji yote ya familia, kama hayupo mtu wa kuhakikisha yale mahitaji yanafanya kile kilichokusudiwa lazima familia itayumba” alisema CPA Philip kwa msisitizo.
Akiongelea nafasi ya mwanamke katika uchumi wa familia na jamii aliitaja kuwa ni kubwa. “Eneo la uchumi, mwanamke anafanya kazi kubwa sana, ukiangalia hata ile kaulimbiu ya mwaka huu inamtaja mwanamke ni mbunifu sana ukilinganisha na mwanaume. Mfano, nchini wajasiriamali wengi ni wanawake. Wajasiriamali hao wanabuni na kutengeneza vitu ambavyo vinachangia kwenye uchumi wa nchi. Pamoja na kwamba wapo wajasiriamali wanaume ila kwa idadi huwezi kuwalinganisha na wanawake, wanawake ni wengi zaidi” alisema nguli huyo wa uhasibu na fedha.
Kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani Mkoa wa Dodoma kitafanyika katika Halmashauri ya Kondoa Mji wilayani Kondoa yakiongozwa na kaulimbiu isemayo “ubunifu na mabadiliko ya teknolojia; chachu katika kuleta usawa wa kijinsi”.