Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WANAWAKE katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kutumia ubunifu na teknolojia katika shughuli za uchumi wa viwanda vidogo na ulipaji wa kodi na tozo za halmashauri katika kuleta maendeleo ya familia na taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkaguzi wa Ndani katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, CPA Jestina Naftal alipokuwa akiongelea umuhimu wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ofisini kwake jana.
CPA Naftal alisema kuwa siku ya wanawake duniani ni muhimu kwa sababu inawakutanisha wanawake kujadili mafanikio na changamoto zinazowakabili. “Wito wangu kwa wanawake, tutumie teknolojia na ubunifu katika kuingia kwenye uchumi wa viwanda vidogovidogo na kuleta maendeleo ya familia na taifa. Wanawake wanaweza kutangaza bidhaa zao walizobuni kwenye mitandao ya kijamii kwa muda mfupi bila kuingia gharama za kusafiri. Muhimu zaidi teknolojia inasaidia kujifunza na kufundisha wengine namna ya kutengeneza bidhaa bora na zenye kuvutia kwenye soko la kitaifa na kimataifa” alisema CPA Naftal.
Maeneo mengine ambayo aliwashauri wanawake kutumia teknolojia na ubunifu ni kupata elimu na kushiriki makongamano ya fursa za kiuchumi. “Teknolojia itumike kuwezesha upatikanaji wa elimu mbalimbali kwa gharama nafuu huku mwanamke akiendelea na shughuli zake za kila siku. Hivyo, teknolojia inawasaidia wanawake kushiriki makongamano mbalimbali bila hata kusafiri kwasababu wanaweza kushiriki kwa njia ya ‘zoom’, ‘webinar’ na mitandao mingine mbalimbali” alisema.
Aidha, aliwataka wanawake kuwa mstari wa mbele katika kulipa kodi na tozo mbalimbali za halmashauri ili wawe mfano wa kuigwa.
“Wanawake wamekuwa waaminifu sana katika kutekeleza maelekezo ya serikali. Nitumie nafasi hii kuwahimiza kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kulipa leseni za biashara na kodi mbalimbali za halmashauri ili waweze kufanya shughuli zao kwa mujibu wa sheria za nchi” alisisitiza CPA Naftal.